Ujerumani kuelekeza mabilioni ya yuro katika jeshi
10 Machi 2025Serikali ya Ujerumani, inayotazamiwa kuongozwa na vyama vya CDU/CSU na SPD, inapanga kutumia mabilioni ya euro kuboresha jeshi la Bundeswehr na miundombinu ya taifa.
Ili kufanikisha hili, wanapendekeza kuondoa vikwazo vya deni kwa matumizi ya ulinzi na kuanzisha mfuko maalum wa miundombinu wa euro bilioni 500.
Katika mazungumzo ya awali ya kuunda serikali, vyama hivyo viligundua kuwa angalau euro bilioni 130 zitakosekana katika bajeti ya miaka minne ijayo. Hii imewafanya viongozi wa kisiasa kutafuta njia mbadala za kupata fedha, ikiwemo kuongeza madeni kwa miradi maalum.
Wachumi wa Ujerumani wamekadiria kuwa Bundeswehr inahitaji euro bilioni 400 kwa miaka ijayo ili kuimarisha jeshi lake. Wakati huo huo, kiasi cha euro bilioni 500 kinahitajika kukarabati barabara, madaraja na miundombinu mingine muhimu nchini.
Soma pia:Chama cha SPD chaunga mkono kushirikiana na CDU/CSU kuunda serikali ya pamoja
Kiongozi wa CDU, Friedrich Merz, ametangaza kuwa matumizi yote ya ulinzi yanayozidi asilimia moja ya pato la taifa hayatazingatiwa chini ya sheria ya kudhibiti deni. Alisema kuwa Ujerumani inapaswa kuwekeza vyovyote inavyohitajika katika ulinzi wake.
''Sisi, makundi ya wabunge wa CDU/CSU na SPD, kwa hivyo tutawasilisha ombi katika Bundestag la kubadilisha katiba ili matumizi ya lazima ya ulinzi katika bajeti ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, ambayo yanazidi kiasi kinachowakilisha asilimia 1 ya Pato la Taifa (GDP), yaondolewe kwenye vikwazo vya ukomo wa deni.''
SPD nayo imependekeza kuanzisha mfuko maalum wa euro bilioni 500 wa miundombinu kwa kipindi cha miaka kumi, ambapo euro bilioni 100 zitapelekwa kwa majimbo ya Ujerumani.
Udhibiti wa deni la taifa
Mabadiliko ya sheria ya kudhibiti deni yatayapa majimbo uwezo wa kukopa kwa kiwango kidogo, jambo ambalo hapo awali liliruhusiwa kwa serikali kuu pekee.
Wabunge wa CDU/CSU na SPD wanatarajia kuwasilisha mabadiliko ya katiba ili kuruhusu matumizi haya makubwa ya fedha. Ili kupitisha marekebisho haya, wanahitaji uungwaji mkono wa theluthi mbili ya Bunge, huku chama cha Kijani kikiwa tayari kuunga mkono mpango huo.
Wataalamu wanahoji jinsi mabilioni haya yatakavyopatikana, kwani tayari Ujerumani ina deni kubwa. Serikali imekuwa ikitumia "mfuko maalum" kama njia ya kukwepa sheria ya kudhibiti deni, lakini wakaguzi wa bajeti wanatahadharisha kuwa hii ni sawa na kuongeza deni kwa mlango wa nyuma.
Ujerumani imekuwa ikitumia fedha maalum kwa miongo kadhaa, kuanzia msaada wa Marshall Plan baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, hadi mfuko wa euro bilioni 100 wa kuongeza bajeti ya Bundeswehr mwaka 2022.
Soma pia:Ujerumani yawasilisha ombi la Euro 2029 kwa wanawake
Hata hivyo, deni linaendelea kukua, na matumizi haya mapya yanaweza kuongeza mzigo wa kifedha kwa vizazi vijavyo.
Wataalamu wa uchumi na sheria wanatahadharisha kuwa kuendelea kuongeza madeni kunaweza kuongeza gharama za riba na kupunguza uwezo wa serikali kufadhili miradi mingine muhimu.
Tayari, Ujerumani inatumia mabilioni ya euro kulipa riba za madeni yake, hali inayoweza kuzidisha mgogoro wa kifedha katika miaka ijayo.
Je, mpango huu utaimarisha uchumi wa Ujerumani au utaongeza changamoto za kifedha kwa taifa? Hilo ni swali ambalo litajadiliwa kwa kina katika siku zijazo.