Ujerumani: Jeshi lina chembe chembe za siasa kali
26 Agosti 2025Jeshi hilo pia limechukua hatua dhidi ya wanajeshi wengine sita walionesha mienendo ya siasa kali. Wizara ya ulinzi Ujerumani ambayo ilikuwa ikijibu maswali kwenye uchunguzi wa kamati ya bunge kutoka kwa wanachama wa chama cha mrengo wa kushoto, imesema mwaka jana jumla ya matukio 280 ya misimamo mikali yalithibitishwa katika nafasi za juu za jeshi, hii ikiwa ni idadi ya juu zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita, iliyoshuhudia visa 205.
Uchunguzi uliofanyika kwa miaka yote miwili, mwaka uliopita na mwaka juzi, ulionesha kuwa wanajeshi kadhaa hawakuadhibiwa kwa makosa waliyoyafanya yanayodaiwa kuendana na tabia za makundi ya misimamo mikali ya mrengo wa kulia.
Wizara ya ulinzi imesema tabia hizo ni pamoja na kuonesha ishara au saluti ya Kiongozi wa zamani wa manazi wa Ujerumani Adolf Hitler, kuimba nyimbo za kibaguzi au kutoa taarifa na kusema maneno yanayoonesha chuki dhidi ya wayahudi au zile za ujamaa.
Hatua zilizochukuliwa baada ya uchunguzi kufanyika, ni pamoja na wanajeshi 72 kuondolewa jeshini mwaka 2023 waliohusishwa na matukio hayo.
Lakini wizara ya ulinzi imesema matukio haya ni madogo mno ukiyalinganisha na idadi ya wafanyakazi katika jeshi hilo la Ujerumani.
Wizara imesisitiza pia kuwa tukio moja linaloonyesha misimamo ya itikadi kali ni kubwa na halipaswi kupuuziwa. Jeshi la Ujerumani kwa sasa lina wanajeshi takriban 260,000 wakiwemo wanajeshi wa kike na wa kiume.