Berlin haitotoa visa kwa walio hatarini kuandamwa na Taliban
1 Septemba 2025Katika hatua ya kupunguza kiwango cha wahamiaji Ujerumani, utawala wa kansela wa taifa hilo umesitisha mipango ya kuwapa hifadhi mamia ya Waafghani, ambao awali waliarifiwa kuhusu utayari wa serikali hiyo kuwakubali kutokana na hatua ya Taliban kurejea madarakani mwaka 2021.
Baadhi ya raia hao walisubiri hatma yao kutoka kwa serikali ya Ujerumani kwa miaka kadhaa wakiwa Pakistan, kabla ya kurejeshwa Afghanistan mapema mwaka huu. Hata hivyo Mahakama ya juu mjini Berlin na Brandenburg imegundua kuwa Ujerumani hailazimiki kisheria kuwachukua raia hao, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa mahakama hiyo.
Kesi hii inajiri baada ya aliyekuwa jaji wa ngazi ya juu nchini Afghanistan, mkewe na watoto wao wanne ambao maombi yao ya visa yalikataliwa mapema mwaka huu, kufuatia uamuzi huo wa serikali ya Ujerumani. Raia wengi wa Afghanistan walioathirika na uamuzi huu wanaaminika kufika mahakamani kupinga uamuzi wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani.
Awali Wadephul na Dobrindt walidaiwa kushindwa kuwalinda wahamiaji
Hata hivyo Ofisi ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema inawasiliana na watu 210 waliorejeshwa Afghanistan. Kando na hayo raia wengine wa taifa hilo la bara Asia ambao maombi yao yalifanikiwa kupita wanatarajiwa kuwasili Ujerumani hii leo usiku (01.09.2025) kutokea Islamabad, Pakistan.
Mapema mwezi Agosti, shirika la kutetea haki za binaadamu la Pro Asyl lilifungua kesi dhidi ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani pamoja na mwenzake wa mambo ya ndani kwa kushindwa kulinda haki za wahamiaji.
Shirika hilo lilisema Johann Wadephul na mwenzake Alexander Dobrindt walishindwa kuwalinda wahamiaji wa Afghanistan waliokuwa na hadhi ya uhakika ya kulindwa nchini Ujerumani.
Hayo yalitokana na taarifa kwamba, serikali ya Pakistan imekuwa ikiwatuma raia wa Afganistan walio na hadhi hiyo ya kulindwa kwa serikali inayoongozwa na Taliban walioitoroka.