Ujerumani inapigia tena kura mageuzi ya sheria ya uhamiaji
31 Januari 2025Hoja hiyo iliyowasilishwa na kiongozi wa Chama cha kihafidhina cha CDU Friedrich Merz Jumatano ilipitishwa na kuungwa mkono na chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD hatua ambayo imeibua hasira kubwa miongoni mwa Wajerumani.
Bunge la Ujerumani linaupigia kura muswada huo uliowasilishwa na muungano wa vyama vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU wiki kadhaa kabla ya uchaguzi wa mapema utakaofanyika Februari 23.
Tofauti na kura ambayo haina uzito kisheria iliyopigwa Jumatano na kuipitisha hoja ya mabadiliko ya sheria ya uhamiaji kwa tofauti ndogo ya kura 348 dhidi ya 345, hoja ya sasa ina maelezo ya kina inayoitwa Sheria ya Udhibiti wa Uhamiaji.
Soma zaidi: Bunge lapitisha mpango wa kuwakataa wakimbizi wengi zaidi mipakani Ujerumani
Inajumuisha kusitisha kitendo cha wakimbizi kuungana na familia zao Ujerumani na inawapa nguvu zaidi maafisa wa uhamiaji kuwarejesha makwao wahamiaji walio mpakani.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kimeashiria kuwa kitauunga mkono muswada huo asambamba na chama cha Free Democratic na chama cha kizalendo cha Sarah Wagenknecht. Katika siku za hivi karibuni hofu imetanda kote Ujerumani kuwa, huenda sasa kukawa na ushirikiano kati ya vyama vikuu vya kisiasa na AfD.
Merz atetea mpango wake licha ya ukosoaji
Licha ya kukosolewa vikali ikiwemo na aliyekuwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Kiongozi wa chama cha CDU Friedrich Merz ambaye ndiye aliyeanzisha hoja hiyo inayopigiwa kura kuwa sheria, ameutetea mpango wake na kusema kuwa, "Tumekuwa na wahamiaji kwa zaidi ya miaka 100. Ujerumani ni nchi ya uhamiaji na tutaendelea kuwa hivyo, lakini ni lazima tuhakikishe kuwa uhamiaji unafanyika katika soko la ajira, kwenye jamii na si uhamiaji ambao unakuwa kitisho katika mifumo ya usalama wa jamii ."
Chama cha AfD ambacho kinashika nafasi ya pili katika utafiti wa maoni ya wapiga kura baada ya chama cha Merz, kinafuatiliwa kwa karibu na mashirika ya ujasusi ya ndani ya Ujerumani kwa kushukiwa kuwa na siasa kali za mrengo wa kulia kupita kiasi.
Maelfu ya watu waliandamana jana Alhamisi kote nchini humo, wakiipinga kura ya kuiunga mkono hoja iliyopitishwa Jumatano kwa ushirikiano mkubwa kati ya Vyama vya CSU/CDU na AfD iliyotaka sheria kali zaidi dhidi ya wahamiaji.
Sehemu ya maandamano hayo ilifanyika mbele ya majengo ya vyama hivyo, yakiwemo makao makuu. Polisi mjini Berlin wanakadiria kuwa watu wasiopungua 6,000 walishiriki kwenye maandamano hayo yaliyokuwa ya amani.