Ujerumani imeiahidi Ukraine uungaji mkono mkubwa Ukraine
28 Mei 2025Ziara hiyo ya rais Volodymyr Zelensky mjini Berlin ni ya tatu tangu ulipofanyika uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwanzoni mwa mwaka 2022. Zelensky amekutana na Kansela Friedrich Merz huku akiwa na lengo la kutafuta hasa msaada wa kijeshi chini ya kiwingu cha kuongezeka mashambulizi ya Urusi dhidi ya nchi yake Ukraine, licha ya kuwepo juhudi zinazoongozwa na Marekani za kumaliza vita.Kansela Merz amemuahidi Zelensky kwamba Ujerumani itampa msaada wa kupambana na Urusi.
Kansela Merz amenukuliwa akisema "Mawaziri wa ulinzi wa nchi zetu hivi leo watasaini mkataba wa maelewano kuhusu kuisadia Ukraine kuunda makombora yake yenyewe ya masafa marefu .Hakutokuweko na vizingiti vyoyote.Na hili litaiwezesha Ukraine kuwa na uwezo wa kujilinda yenyewe hata dhidi ya jeshi lake nje ya ardhi yake. Huu utakuwa mwanzo wa mpango mpya wa mashirikiano ya kijeshi kati ya mataifa yetu mawili,ushirikiano unaoweza kuwa na mafanikio makubwa.'' Alisema Kansela huyo mpya.
Merz amekataa kuzungumzia Ujerumani kupeleka silaha nzito Ukraine
Pamoja na kutowa ahadi hiyo Merz amekataa kuzungumzia ikiwa binafsi ataruhusu kupelekwa kwa makombora ya kimamboleo ya masafa marefu ya Taurus nchini Ukraine.
Hata hivyo kwenye mkutano wao na waandishi wa habari, Zelensky hakusita kutaja wazi wazi kwamba nchi yake bado inatarajia kwamba Ujerumani itaipatia makombora hayo ya masafa marefu. Itakumbukwa kwamba mtangulizi wa Kansela Merz, Olaf Scholz alikataa katakata pendekezo hilo la Ukraine huku upande mwingine Moscow ikiionya Ujerumani mara kwa mara kutothubutu kuipatia Ukraine makombora hayo.
Soma zaidi:Urusi yaishambulia Kyiv kwa mabomu na droni
Ziara ya Zelensky mjini Berlin, imekuja siku chache baada ya Urusi kuanzisha kampeini kubwa ya kuishambulia Ukraine kwa makombora na droni na pia katika wakati rais wa Marekani Donald Trump akionesha kuchoshwa na vitendo vya rais wa Urusi Vladmir Putin.Merz ameahidi kwamba serikali yake haitoacha kuishinikiza Urusi. Zaine amesema "Tutaendelea kuongeza shinikiza dhidi ya Urusi.Tunafanya hivyo ili kuudhifisha uwezo wa kijeshi wa Moscow.Lakini tunafanya hivyopia ili kufungua njia ya kufanyika mazungumzo. Kwetu sisi Ujerumani nasema hivi kwa kuweka wazi kwamba tutafanya kila tuwezalo kuzuia kufanya kazi tena, bomba la usafirishaji gesi la Nordstream 2.'' Alisema Kansela.
Ujerumani pia itaipatia msaada wa ziada wa takriban yuro bilioni 5 Ukraine kwa mujibu wa wizara ya ulinzi kufuatia ziara hiyo ya Zelensky Berlin. Zelensky atakutana pia na rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir katika kasri la Bellevue.