"Ujerumani ifikirie kuwaondosha wanajeshi wake"
30 Mei 2006La kwanza ni gazeti la “Landeszeitung” la mjini Lüneburg linaloandika yafuatayo:
“Kwa upande mmoja unaweza kusema: Nchi za Magharibi zimeshindwa. Mamillioni ya dola za msaada wa kuijenga upya Afghanistan zimepotea. Vyovyote vile, dunia imeangalia Irak tu. Lakini kwa upande mwingine inaonekana kwamba nchi zimejiharibia kwa kutaka kufanya kupita kiasi. Nchi ya Afghanistan yenye makabila mengi haifai kuweka mfano wa kujenga demokrasia. Mara moja tu makabila yote yalikubaliana katika historia, yaani wakati wa kuwafukuza Warusi waliomiliki nchi yao. Sasa viongozi wa waasi wanakubaliana kuzisimamisha nchi za Magharibi katika kuleta demokrasia Afghanistan ambapo tangu zamani viongozi wa makabila wanahusishwa na mamlaka ya kisiasa.”
Gazeti la “Märkische Oderzeitung” lina wasiwasi zaidi likiandika:
“Sasa mkakati mzima wa nchi za kimataifa kujenga demokrasia na hivyo kuleta hali bora ya maisha unakabiliwa na hatari ya kuleta fujo tu. Waasi na wanabiashara ya dawa za kulevya wanaongeza jitihada zao za kupiga vita wanajeshi wa kutoka nje. Wakati huo huo serikali ya Ujerumani inasisitiza usalama na amani itakuwepo nchini Afghanistan baada ya muda mfupi. Lakini ukiangalia hali inaendelea vipi sasa hivi, inaonekana muda wa kuleta amani umekwisha.” - Haya ni maoni ya “Märkische Oderzeitung”.
Gazeti la “Neues Deutschland” la kutoka Berlin linalinganisha hali ya Afghanistan na ile ya nchini Iraq. Limeandika:
“Katika kivuli cha hali mbaya zaidi nchini Iraq, usalama usioimarishwa nchini Afghanistan unavunjika. Idadi ya watu wanaojitoa mhanga na kujiripua inazidi kuongezeka, na tangu wiki kadhaa zilizopita Wataliban wanalishambulia eneo la Kusini la Afghanistan. Marekani inayajibu mashambulio haya kwa kutumia mabomu bila ya kujali athari kwa watu wa kawaida. Kwa hiyo, vita vinaendelea miaka mitano baada ya Wataliban kuondolewa madarakani.”
Na mwishowe tunalinukuu gazeti la “Braunschweiger Zeitung”:
“Ghasia zinazotokea mjini Kabul vile vile ni ishara kwa jeshi la Ujerumani Bundeswehr. Bila shaka kuna urafiki kati ya Wajerumani na Waafghanistan uliojengwa katika miaka mingi. Lakini urafiki huo hauwezi kuzuia uchuki na mashambulio. Ni wazi kwamba kupingwa wanajeshi wa kutoka nje kunawahusu wageni wote. Kwa hivyo serikali ya Ujerumani ifikirie kuwaondosha wanajeshi wake kabla ya wao kushambuliwa pia.”