Ujerumani haiko tayari kuitambua Palestina kama dola huru
29 Julai 2025Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Berlin pamoja na Mfalme Abdullah II wa Jordan, Kansela Merz alisema anaamini kuwa suluhisho la mataifa mawili linaendelea kuwa njia bora zaidi ya kufikia amani ya kudumu. Lakini akasema hali ya kulitambua taifa la Palestina si hatua sahihi kwa sasa. Merz ameongeza kuwa huenda hilo likawa mojawapo ya hatua za mwisho katika mchakato mzima wa suluhisho la mataifa mawili.
Hata hivyo, Merz ametangaza kuwa ndege mbili aina ya A400M kutoka Ujerumani tayari zipo njiani kuelekea Jordan kwa ajili ya kushiriki katika shughuli za kudondosha misaada ya kibinadamu kwa njia ya anga katika Ukanda wa Gaza. Ndege hizo zitapakia misaada nchini Jordan na zinatarajiwa kuanza kazi hiyo mwishoni mwa wiki hii, au hata kuanzia kesho Jumatano, kwa ushirikiano na Ufaransa na Jordan.
Mashirika ya haki za binaadamu ya Israel yazungumzia mauaji ya kimbari Gaza
Kwa upande wake, Mfalme Abdullah II wa Jordan ameleezea furaha yake kwa msaada huo lakini akaonya kuwa misaada ya anga haiwezi kutosha.
"Vita ya Israel dhidi ya Gaza lazima visimame. Janga la kibinadamu linazidi kuwa kubwa mno. Picha za watoto wanaokufa kwa njaa Gaza zimetikisa dhamira ya watu duniani kote. Ni doa kwa ubinadamu wetu wa pamoja kuruhusu hili kuendelea," alisema Mfalme Abdullah.
Merz pia amesema Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinapanga kuwatuma mawaziri wao wa mambo ya nje nchini Israel wiki ijayo ili kuwasilisha msimamo wa pamoja wa nchi hizo tatu kuhusu hali ya Gaza. Katika wiki za hivi karibuni, nchi hizo tatu zimesisitiza haja ya kusitishwa kwa janga la kibinadamu Gaza na kutoa wito wa kuruhusu misaada zaidi kuingia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa pia alithibitisha kwamba Paris itashiriki katika shughuli za angani kusaidia watu wa Gaza, lakini ikasisitiza kuwa njia bora zaidi ni kufunguliwa kwa vivuko vya ardhini ili misaada iweze kuingia kwa wingi zaidi.
Umoja wa Mataifa wajadili suluhisho la mataifa mawili huru
Wakati hayo yakiendelea, shirika la kimataifa linalofuatilia usalama wa chakula duniani — IPC — limetoa tahadhari kuwa hali ya njaa ya kiwango cha janga inainyemelea Gaza, likieleza kuwa "vifo kwa wingi" vinatarajiwa bila hatua za dharura.
Taarifa hiyo imekuja kufuatia picha za watoto waliodhoofika na ripoti za vifo vinavyohusishwa na njaa, huku Umoja wa Mataifa ukisema hatua za Israel za kufungua njia salama bado hazitoshi, na malori ya misaada yanaporwa kabla hayajafika kwa walengwa.
Takwimu za Wizara ya Afya ya Gaza, inayodhibitiwa na Hamas, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 60,000 wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo, kufuatia shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.