Ujerumani bado haina serikali
20 Septemba 2005Berlin:
Undaji wa serikali mpya ya Ujerumani huenda ukachukua juma moja baada ya uchaguzi mkuu uliofanywa juzi Jumapili na kusababisha hakuna aliyeshinda wala kushindwa. Wagombea wote wawili wa wadhifa wa ukansela, Bibi Angela Merkel wa vyama ndugu vya upinzani vya CDU/CSU na Kansela wa sasa hivi Gerhard Schröder wa chama tawala cha SPD, wanadai haki ya kuunda serikali mpya. Vyama hivi vimetangaza kuwa vitaanzisha mazungumzo na vyama vingine kwa lengo la kuunda serikali ya muungano isipokuwa chama cha mrengo wa kushoto. Wanasiasa wengi wa vyama vya CDU/CSU wanazungumzia uwezekano wa kuundwa serikali ya mseto na vyama vya FDP na Walinzi wa Mazingiza. Chama cha Kijani bado hakijaafiki muungano kama huo. Chama cha FDP nacho kinakataa kuungana na SPD. Vyama vya CDU/CSU, kwa mujibu wa matokeo rasmi, vimepata viti 225 na Chama cha SPD kina upungufu wa viti vitatu. Kwa vile vyama vya CDU/CSU havina wingi mkubwa haviwezi kuunda serikali peke yao.