Uingereza yatishia kuikatia misaada Rwanda kwa yajiriyo Goma
30 Januari 2025Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza, David Lammy, aliliambia bunge kwamba Rwanda inapokea msaada wa zaidi ya dola bilioni moja kila mwaka kutoka jumuiya ya kimataifa, zikiwemo takribani dola milioni 40 kutoka Uingereza, lakini "misaada yote hiyo sasa iko hatarini kukatishwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya majirani wa Rwanda."
"Sisi kwenye bunge hili tunaweka wazi kwamba hatuwezi kuwa na nchi ambazo zinatishia heshima na mamlaka ya nchi nyengine. Kama ambavyo hatuwezi kuvumilia hilo kwenye bara la Ulaya, hatuwezi kulivumilia pia popote pengine linapotokea duniani." Alisema Lammy.
Soma zaidi: Kiongozi wa DRC asema jeshi lake linapambana vikali dhidi ya mashambulizi ya M23
Msimamo huu wa Uingereza unafuatiwa na ule wa Ujerumani na Marekani ambazo kwa pamoja zimeeleza wasiwasi wao juu ya uungaji mkono wa Rwanda kwa kundi la waasi la M23, ambalo kwa sasa linadhibiti sehemu kubwa na muhimu za mashariki mwa Kongo, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini na rasilimali nyengine.
Kagame aijia juu Afrika Kusini
Katika kile kinachoonekana kama muelekeo wa vita hivyo kugeuka kuwa vya kikanda, Rais Paul Kagame wa Rwanda alitoa kauli kali siku ya Alkhamis (Januari 30) dhidi ya uwepo wa vikosi vya jeshi ya Afrika Kusini kwenye eneo la mashariki mwa Kongo, akisema jeshi hilo halina nafasi yoyote hapo na kwamba nchi yake iko tayari kukabiliana na chochote kutoka Pretoria.
Tayari wanajeshi 13 wa Afrika Kusini wameshauawa kuanzia wiki iliyopita hadi sasa wakiwa kwenye makabiliano na wapiganaji wa M23 wanaoendelea kuyatwaa maeneo kadhaa mashariki mwa Kongo.
Soma zaidi: Duru: Waasi wa M23 waanza kuelekea Bukavu
Kwenye mkutano ulioitishwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais William Ruto wa Kenya, siku ya Jumatano (Januari 29), Kagame aliweka wazi kwamba nchi yake haitaweza kuyumbishwa kwenye msimamo wake juu ya kile kinachoendelea kwenye eneo hilo, huku akiilaumu jumuiya hiyo kushindwa kuwa na meno, wakati Kinshasa ikitengeneza matatizo kwa kila upande.
"Nilijuwa mgogoro huu utafikia kiwango hiki kwa sababu nilikuwa sioni mtu anayebeba dhamana ya kuyasimamia mambo wakati yakienda kombo. Kwa hili ningetaka kuiuliza jumuiya yetu wenyewe, kipi tulichokuwa tunakitaka mwanzoni, tulifanya nini kukipata, tunafanya nini sasa na tutafanya nini kwa baadaye. Niliuliza kwenye mkutano wa mwisho wa kilele, iko wapi Jumuiya ya Afrika Mashariki na kweli inajuwa ikitakacho?" Alisema Kagame kwenye mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Soma zaidi: Marekani yaitaka Rwanda kujiondoa katika mji wa Goma
Hata hivyo, Rais Felix Tshisekedi wa Kongo hakuhudhuria mkutano huo wa viongozi wakuu wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Badala yake, alihutubia taifa jioni ya Jumatano ambapo alisema jeshi la nchi yake lilikuwa tayari kupambana na kurejesha kila kipande cha ardhi kilichotwaliwa na wapiganaji wa waasi.