Uingereza yafadhili waathiriwa wa tetemeko Afghanistan
2 Septemba 2025Tetemeko hilo ambalo limeikumba jimbo la Kunar, limesababisha vifo vya zaidi ya watu 800 na kuwajeruhi maelfu ya wengine, na kuacha mamia makaazi rasmi na huduma za msingi.
Msaada huo utatolewa kupitia mashirika mawili makuu - shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu UNFPA na shirika la Msalaba Mwekundu wa Kimataifa IFRC. Fedha hizo zitagawanywa kwa usawa kati ya mashirika hayo ili kuwezesha utoaji wa huduma za afya, vifaa vya dharura, na mahitaji ya msingi kwa waathiriwa wa tetemeko hilo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy ameeleza masikitiko yake kufuatia tetemeko hilo la ardhi na kuongeza kwamba Uingereza itasimama pamoja na raia wa Afghanistan katika kipindi hiki kigumu.
Amesisitiza kuwa msaada huo ni sehemu ya dhamira ya Uingereza ya kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na majanga ya kibinadamu.
Hata hivyo, changamoto za kijiografia na hali mbaya ya hewa zimeathiri juhudi za kufikisha msaada. Eneo la milima pamoja na mafuriko ya hivi karibuni yamezuia upatikanaji wa maeneo mengi yaliyoathirika na kuongeza ugumu katika utoaji wa misaada.
Kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya misaada, zaidi ya watu milioni 23 nchini Afghanistan wanaripotiwa kuhitaji msaada wa kibinadamu.