Uingereza yasitisha msaada kwa Rwanda kutokana na vita DRC
26 Februari 2025Vikosi vya Burundi ambao ni washirika wa serikali ya Kinshasa vinaendelea kupelekwa mashariki mwa Kongo, huku Uingereza ikitangaza kusitisha msaada wake wa moja kwa moja kwa Rwanda kutokana na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23 ambao wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema wanaungwa mkono na Rwanda.
Msemaji wa serikali ya Uingereza amesema, "Rwanda huenda ina wasiwasi kuhusu usalama wake, lakini haikubaliki kutatua hali hiyo kwa njia ya kijeshi. Suluhisho la mgogoro huu ni la kisiasa pekee."
Soma pia: Zaidi ya watu 7,000 wauawa kutokana na machafuko nchini Kongo
Msemaji huyo ameongeza kuwa, msaada kwenda Kigali utasitishwa mpaka kupatikane kile alichokiita "maendeleo makubwa” katika kupunguza mapigano.
Rwanda hata hivyo imejibu na kuutaja uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kusitisha misaada kama "adhabu".
Maelfu ya raia wakimbia makaazi yao
Tangazo hilo la kusitisha misaada kwenda Rwanda limetolewa baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy kufanya mkutano wiki iliyopita na Rais wa Rwanda Paul Kagame mjini Kigali na baadaye kukutana na Rais wa Kongo Felix Tshisekedi mjini Kinshasa.
M23 imechukua udhibiti wa miji mikubwa miwili mashariki mwa Kongo katika wiki za hivi karibuni, na hivyo kuwa na udhibiti wa eneo kubwa lenye utajiri wa madini tangu kundi hilo lilipoanza tena mapigano mwishoni mwa mwaka 2021.
Wapiganaji wa M23 waliuteka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini wa Bukavu wiki iliyopita. Hiyo ni baada ya kuuteka mji wa Goma, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini na jiji kubwa mashariki mwa Kongo mwishoni mwa mwezi uliopita.
Soma pia: Kabila amsuta Rais Tshisekedi kuhusu mzozo mashariki mwa Kongo
Kundi hilo limeendelea kusonga mbele kwa urahisi katika eneo hilo bila ya upinzani wowote kutoka kwa jeshi la serikali ya Kongo.
Wapiganaji wa M23 walikuwa wakielekea katika mji wa Uvira, ambao upo karibu na eneo la kaskazini magharibi mwa Ziwa Tangayika, mkabala na Bujumbura, mji mkuu wa kiuchumi wa Burundi.
Vikosi vya Burundi vinaripotiwa pia kuelekea kaskazini mwa Uvira ili kuwazuia wapiganaji wa M23.
Viongozi wa zamani wateuliwa kuongoza mchakato wa amani
Wapiganaji wa kundi la Wazalendo, wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya Kongo, wameungana na vikosi vya Burundi katika eneo la Luvungi. Wapiganaji wa M23 wameonekana pia karibu na mji wa Kamanyola, takriban kilomita 75 kaskazini mwa Uvira.
Hayo yanatokea wakati jumuiya mbili za kikanda barani Afrika zikiteua jopo la viongozi watatu wa zamani kusimamia juhudi za kupatikana amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia: UN yaonya kuhusu kusonga mbele kwa M23 Kongo
Jumuiya mbili za kikanda – Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC – zimeungana katika wiki za hivi karibuni katika juhudi za kusitisha mapigano.
Jumuiya hizo mbili zilitangaza mapema wiki hii kwamba rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta, Waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia Hailemariam Desalegn na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo wameteuliwa kusimamia mchakato mpya wa amani Kongo.
EAC na SADC walikubaliana katika mkutano wa kilele uliofanyika mnamo Februari 8 kuunganisha michakato miwili tofauti ya amani – wa Luanda na Nairobi – iliyokuwa inaendelea kabla ya kuongezeka kwa ghasia hivi karibuni.
Wakati huo huo, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Karim Khan akiwasili Kongo kuchunguza matukio ya ongezeko la ghasia.
Khan amewaambia waandishi wa habari baada ya kuwasili mji mkuu wa Kinshasa kwamba, wanatiwa wasiwasi na matukio ya hivi karibuni yanayoendelea Kongo na anafahamu kwamba hali mashariki mwa nchi hiyo ni mbaya.
Mwendesha mashtaka huyo wa ICC amesema, "Ujumbe unapaswa kufikishwa kwa uwazi, kuwa kundi au jeshi lolote lenye silaha, ama washirika wao hawana kibali cha kufanya watakavyo."