Uingereza na Ujerumani wasaini mkataba wa kuimarisha ulinzi
18 Julai 2025Mataifa hayo ya Ulaya yanajaribu kuilinda Ukraine na kujilinda wenyewe dhidi ya Urusi yenye msimamo mkali, hasa katika wakati ambapo msaada kutoka kwa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani umekuwa wa mashaka.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na Starmer, Kansela Merz aliyasifia makubaliano hayo kuwa ya kihistoria:
"Hii ni siku ya kihistoria kwa mahusiano kati ya Ujerumani na Uingereza. Tunataka kushirikiana kwa karibu zaidi, hasa baada ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya. Tumekuwa tukichelewa sana kuhitimisha mkataba wa aina hii kati yetu. Tunataka kushirikiana kwa karibu zaidi katika maeneo ya ulinzi, sera za kigeni, pamoja na sera za kiuchumi na za ndani. Kuna maeneo mengi sana ambapo Uingereza na sisi tunaweza kushirikiana kwa karibu zaidi — kuliko ilivyokuwa hapo awali."
Viongozi hao wawili pia walijadili kwa kina mipango ya kuitumia silaha zaidi Ukraine, hasa baada ya rais Donald Trump wa Marekani kuashiria kwamba ataziuzia nchi za Jumuiya ya NATO silaha ikiwemo mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot ambayo Kyiv imekuwa ikiihitaji.
Ziara ya Merz inajiri wiki moja baada ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nchini Uingereza huku Kansela Merz akitarajiwa kuwa mwenyeji wa Macron mapema wiki ijayo.