Uingereza lawamani juu ya mateso ya Mau Mau nchini Kenya
8 Machi 2005Serikali ya Uingereza iliyokuwa mkoloni wa kenya imetakiwa kuomba msamaha kutokana na mateso waliyoyapata wapiganaji wazalendo wa nchi hiyo katika vita vya kujikomboa vya Mau Mau, lakini kampeini za wapiganaji hao wa zamani huenda zikaongeza mgawanyiko miongoni mwa wakenya.
Mwanahistoria wa uingereza,David Anderson ambaye ni mwalimu wa chuo kikuu cha Oxford amechapisha kitabu cha historia ya mwaka huu juu ya ukiukaji wa haki katika mizozo ya miaka ya 1950 amesema mashtaka yeyote yaliyotolewa na wapiganaji hao lazima yawahusu wakenya waliouwawa na mau mau na vilevile mauaji yalioyotekelezwa na waingereza kwa waasi.
Anasema hakuna haja ya kufufuliwa kwa chuki zilizopita,hilo halitamsaidia yeyote,ni muhimu kwa serikali ya Kenya na Uingereza zielewane kwa kile kilichotendeka katika miaka ya 1950.
Wengi wakiwa kutoka kabila la Kikuyu,Mau Mau walianza vita vyao dhidi ya utawala wakikoloni katika mwaka wa 1952. Mashujaa ambao wanaonekana na wakenya kama watetezi wa uhuru wanasema serikali ya Uingereza iliwanyanyasa mashujaa hao kwa kuwafunga ndani ya jela wakiwa wengi,Kuwatesa na kuwapiga.
Lakini mbali ya kuwa ni chama cha vugu vugu la ukombozi nchini Kenya ,Tangu mwaka 1963,Mau mau imekuwa ni suala linalozua mgawanyiko na bado inachukua nafasi kubwa katika historia ya serikali ya Kenya.
Jamii ya wakikuyu nchini Kenya inatambuliwa kwa mgawanyiko kati ya vizazi vilivyozaliwa na wazalendo waliopigania uhuru ambao ndio MauMau na wale waliozaliwa na watiifu wa utawala wa Muingereza.
Wengi wa wapiganaji hao wazalendo sasa wanaishi katika umaskini wa kupindukia, na kamwe hawakupata ardhi waliyoipigania ambayo kwa kiasi kikubwa imegawanywa kwa watiifu wa muingereza waliyempiga vita.
Mwezi uliopita wapiganaji wazalendo wa kenya wa Mau Mau walisema watafungua kesi dhidi ya Uingereza kudai fidia juu ya mateso waliyoyapata chini ya wanajeshi wa Uingereza katika kipindi cha hali ya hatari nchini humo.
Wito wa Mau Mau umeungwa mkono na waziri wa sheria nchini Kenya Kiraitu Murungi huku mtuhumiwa mwenyewe ikiwa ni serikali ya Uingereza ikikataa katakata kutoa sauti yake kuhusu hilo.
Anderson yeye analaumu sera za Uingereza na matendo yake lakini pia anawahurumia waliojikuta chini ya ukoloni wa Muingereza. Anasema kwamba wale waliokuwa watiifu wa Uingereza ilikuwa kutokana na kupinga njia zilizotumiwa na Mau Mau au kwa sababu ya kulazimishwa kula kiapo cha wakikuyu.
Hata hivyo anasema serikali ya Uingereza bora ikubali kosa lake kwa kuomba msamaha wakenya kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu uliotekelezwa na wanajeshi wake enzi za ukoloni na hilo huenda likatuliza kidonda cha wakenya.
Yeye anafikiri huu ndio wakati muhimu kufanya kampeini za mapatano kuliko kuwepo na mvutano.
Katika kitabu chake Anderson anasema Uingereza ilikiuka sheria kuwakandamiza Mau Mau,kuwanyonga wakenya zaidi ya elfu moja kati ya mwaka 1952 na mwaka 1959.