Uingereza kupeleka misaada kwa njia ya anga Gaza
26 Julai 2025Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu Jumamosi na viongozi wa Ufaransa na Ujerumani. Hatua hiyo inafuatia hasira za kimataifa zinazoongezeka kuhusu njaa kali inayowakumba watu wa Gaza.
Huko Gaza, takriban watu 25 wameuawa kutokana na mashambulizi ya anga na risasi za jeshi la Israel usiku wa kuamkia leo Jumamosi. Kwa mujibu wa maafisa wa afya ni kwamba wengi wa waliouawa walikuwa wakisubiri misaada ya chakula karibu na eneo la Zikim kwenye mpaka na Israel.
Huku hayo yakijiri, maafisa wa Hamas wameeleza mshangao wao kufuatia tuhuma za Rais wa Marekani Donald Trump kwamba kundi hilo "halitaki kwa dhati" makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza. Hamas imetupilia mbali tuhuma hizo na kuitaka Marekani kuwa na msimamo wa haki zaidi.