Uhariri wa mazeti ya Ujerumani hii leo:
20 Januari 2004Gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani, SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, kuhusu ziara ya Kansela Gerhard Schröder barani Afrika, linaandika: Mtu asije akatilia chumvi sana ushawishi wa Ujerumani katika nchi za Afrika. Lakini ziara hii ya Kansela Schröder, inakaribishwa sana na vyombo vya habari vya kiafrika, nafasi ambayo Kansela anatumia kwa busara, kusisitiza kile anachomaanisha kuhusu ule anaoutaja "ushirika wa kuaminiana". Na endapo hali ni hivyo, basi licha ya sifa zake kuhusu mipango ya mageuzi barani humo, Kansla pia atabidi kuwa na wakati wa kufanya mazungumzo wazi pamoja na rais wa Afrika ya Kusini Thabo Mbeki. Kwani kinyume cha nchi kama Kenya na Ghana, Rais Mbeki anaendelea kumuunga mkono dikteta wa Zimbabwe. Lakini anakanusha tangu muda mrefu, kuwa na uhusiano naye kwa sababu ya hatima yao ya pamoja ya ugonjwa wa ukimwi. Na endapo Kansela Schröder hatazungumzia swala hili, basi rais Mbeki atahisi kuthibitishwa msimamo wake.
Nalo gazeti la mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Nubrandenburg, NORDKURIER, linadai Ujerumani kuzingatia siasa za haki barani Afrika, linapoandika: Kansela Schröder anasema kweli, anapobainisha kwamba, migogoro ya kimkoa katika nchi za Afrika, haitaweza kutatuliwa, bila ya ushirika wa karibu pamoja na bara jirani yao la ulaya. Inaweza kutumainiwa tu kwamba, ziara ya Kansela pamoja na mameneja wa uchumi wanaoongozana naye barani Afrika, haitatilia uzito pekee ajira rahisi, bali cha mstari wa mbele ni Ujerumani kuzitolea nchi za kiafrika misaada ya kuzisaidia kujimudu. Yote mengine yangesikika kama ni unafiki tu, ambao ungedumu muda mfupi tu na hatimaye kuzusha hasara badala ya kuleta faida.
Gazeti lingine mashuhuri la kusini mwa Ujerumani, FRANKFURTER RUNDSCHAU, leo linatilia uzito mazungumzo yaliyofanyika kati ya mratibu wa hali nchini Irak wa marekani, Paul Bremer, pamoja na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Koffi Annan, kwa kuandika: Inaelekea karibuni itaibidi Marekani kupiga hodi mjini Brussels, kwa nia ya kupata msaada wa kijeshi kutoka shirika la NATo, na wa pesa kutoka umoja wa ulaya. Na endapo umoja wa ulaya hautakuwa na cha kuipatia Marekani, basi utajikuta kwa mara nyingine kuhatarishwa na siasa za Marekani, za kuijenga upya Irak. Yabidi kukumbukwa kwamba, swala muhimu wakati huu nchini Irak, sio ni la kijeshi, bali ni la kisiasa. Kwa hivyo, unaohitajika sasa ni msimamo wa busara wa pamoja kati ya mabwana Schröder, Chirac pamoja na anayejitazama kuwa mtaalamu wa bara la ulaya Bw.Blair, wa kuufanya umoja wa ulaya kuchukua hatua kuelekea masilahi ya Marekani:
Nalo gazeti la mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Potsdam, MÄRKISCHE ALLGEMEINE, kuhusu mada hii linaandika: Kidokezo cha umoja wa mataifa, cha kuharakisha msaada kwa wamerikani, hakina uzito mkubwa hivyo, hasa kwa sababu, kama hali ilivyokuwa wakati uliopita, Marekani haitakuwa tayari kuacha msimamo wa kuwa mshika hatamu kuhusu Irak.
Na katika upande wa pili, mtu hawezi kupuuza nafasi hii, ya mchango ambao umoja wa mataifa ungekuwa tayari kutoa. Yule ambaye ananuwia kushawishi, basi anabidi kutumia fursa hii bila kuchelewa. Umoja wa mataifa hautaki kutumiwa na Bw.Bush katika kampeni zake za uchaguzi ujao wa rais.
Tunakamilisha uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo, kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la MANNHEIMER MORGEN, linapozingatia mtindo wa wale wanaofanya ajira za kukimbia kodi, kwa kuuliza kwanza - je - nini hasa ni maana ya ajira hizi, ambazo mara hazivunji sheria, lakini ambazo ni za usaidiano kwa malipo ya Euro chache tu kila wiki? Kiini cha msako dhidi ya waajiriwa kama hao, hufanyika hasa katika sekta za uashi na utumishi katika mahoteli na mikahawa, kwa sababu wanasababisha hasara ya mabilioni kwa kukimbia malipo ya kodi. Kwa sababu hii, chama mshirika mdogo katika serikali ya Berlin cha Kijani, kinataka kuwahami kwa kila njia, mamilioni ya raia wanaofanya utumishi wa hela chache tu.