Uhariri wa magezeti ya Ujerumani hii leo
30 Desemba 2003Mada muhimu kabisa inayotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo, ni matokeo ya uchaguzi wa bunge katika nchi ya Balkan ya Serbia. Magazeti mengi yanasifu kwa hofu hasa mafanikio ya wanasiasaa wenye kufuata mkondo wa siasa kali. Kuhusu mada hii, gazeti la kusini mwa Ujerumani, STUTTGARTER ZEITUNG, linaandika: Mnamo miaka iliyopita, wanasiasa wa nchi za magharibi, walikuwa na matumaini makubwa ya kupatikana mabadiliko katika eneo la Balkan. Lakini hali ilibadilika haraka sana kwamba, serikali zilizojiwekea mipango ya mageuzi, iwe ni katika Kroatia, Bosnia au Serbia, zilikuwa zikipata pesa za kugharamia mageuzi hayo kutoka nchi za magharibi, iwapo tu serikali za zamani zimeshatimuliwa kabisa. Lakini nchi za magharibi, hazikuwa tayari kubeba muzigo huo wa gharama za mageuzi, ndio maana zilikosa pesa za kugharamia ushawishi wa kisiasa. Si ajabu basi kwamba, wapigaji kura wengi walikwishakatishwa tamaa.
Gazeti la mashariki mwa Ujerumani, LEIPZIGER VOLKSZEITUNG, kuhusu mada hii linasema: Taarifa hii ya mafanikio ya wanasiasa wenye kufuata siasa kali, hapana shaka itamfurahisha sana kiongozi wa zamani wa Serbia, Milosevic bado akiwa kizuizini katika The Hague. Miaka miwili baada ya kufikishwa katika mahakama hiyo ya kimataifa, wenye kufuata siasa kali wa Serbia, wanahisi kuthibitishwa kwa mafanikio yao kwamba, kiongozi wao wa zamani hana hatia ya mashtaka ya kuwa mhalifu wa kivita katika eneo la Balkan, na kwamba hakuwa wa pekee kulaumiwa. Wale waliopoteza ushawihi, ni wafuasi wa waziri-mkuu aliyeuliwa marehemu Djindjic, ambao waliapa kupepea bendera ya kuleta mageuzi ya kisiasa katika Serbia. Lakini hawakufanikiwa katika yale waliyonuwia.
Matokeo haya ya uchaguzi wa bunge katika Serbia, yamezifanya nchi nyingi jirani za ulaya, kushtuka na hata kushindwa kueleza maoni yao, kama gazeti la MÄRKISCHE ODER-ZEITUNG, linavyoandika katika uhariri wake: Mshtuko huu unaeleweka, mtu akipata taarifa kwamba, washtakiwa wawili katika mahakhama ya The Hague, kwa sababu ya uhalifu wa kivita, Vojislav Seselj na Slobodan Milisevic, wanaweza kufanikiwa kujinyakulia asilimia 35 ya kura kwenye uchaguzi huo wa juzi. Nchi jirani pia zinashindwa kueleza misimamo yao, kwa sababu hazijui kwa hakika, namna ya kuipatia misaada nchi hii ya Balkan, kwa nia ya kuwafanya raia kuwa na imani tena katika demokrasia.
Gazeti la mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Rostock, OSTSEE-ZEITUNG, nalo halikadhalika linaona hofu kuhusu matokeo ya uchaguzi huo linapoandika: Ni kama kichekesho kwamba, wanasiasa hawa wenye kufuata siasa kali, wamefanikiwa kujinyakulia viti 81 kutoka jumla ya viti 250 katika bunge. Matokeo haya, yanathibitisha wazi jinsi mkondo wa demokrasia unavyohatarishwa, wakati inapotawala hali ya ukosefu mkubwa wa ajira, umaskini na kutokuweko na matumaini inavyozidi kujitandaza katika maisha ya kila siku ya raia. Isisahauliwe sura nyingine katika uchaguzi huu, kwamba ulishawishiwa sana na hisia za kupinga matakwa ya nchi za magharibi, adhabu dhidi ya masilahi yao katika eneo la Balkan. Kinachotakikana hasa, ni msaada wa kuisaidia nchi hiyo kuhifadhi tena demokrasia, na sio msaada wa kukanyagilia mbali udikteta, ukweli ambao hauihusu serikali ya Belgrade pekee. Kwa sababu hii, ni wajibu muhimu wa umoja wa ulaya, kutoa ishara ya pia kuwaelekeza njia raia wa Serbia. Nalo gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani, FRANKFURTER RUNDSCHAU, linakamilisha mada hii kwa kusema: Mafanikio ya chama cha wenye kufuata siasa kali, yanawafanya wengi kuingiwa na kinyongo. Sababu hasa ni kwa kuwa, kiongozi wake Vojislav Seselj, alijitolea kufikishwa katika mahakhama ya kimataifa katika The Hague, lakini hana haki ya kukalia kiti chochote katika bunge, kabla ya kupitishiwa hatua za adhabu. Hali kama hii, pia inamhusu kiongozi madhubuti kabisa wa zamani wa Serbia Slobodan Milosevic, ambaye chama chake cha kisoshalisti, kilifanikiwa kuvuka kiunzi cha asilimia tano zinazodaiwa pindi kuweza kuingia katika bunge. Inaelekea wanasiaasa hawa wawili wa zamani hawatapata fursa ya kuketi tena katika bunge mjini Belgrade, lakini vyama vyao vitachukua hatua za kuhakikishwa kwamba, Serbia haitakuwa nchi inayotengwa kimataifa.