Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
8 Aprili 2004Gazeti mashuhuri la mji mkuu Berlin, NEUS DEUTSCHLAND, kuhusu hatua iliyochukuliwa na seneta wa Berlin na mwenyekiti wa tawi la chama-tawala SPD, Peter Strieder ya kujiuzulu , kuhusiana na kashfa ya pesa, linaandika: Jana haikuwa siku nzuri kwa serikali ya muungano kati ya vyama vya SPD na PDS mjini Berlin. Muungano huu unakabiliwa na hatari, hata ikiwa unajaribu kujiokoa kwa njia ya kufanya mabadiliko ya viongozi. Bila ya Seneta Strieder, muungano wa vyama hivi unakabiliwa na matatizo makubwa. Ndio maana baada ya kushindwa kubana matumizi katzika nusu ya kwanza ya kipindi cha kuwa madarakani, sasa itaubidi kugeuza mtindo wa kisiasa katika nusu ya pili.
Kuhusu mada hii, gazeti lingine la Berlin, BERLINER KURIER, linaandika: Seneta Peter Strieder kila mara alitaka sana kuwa ni mwanasiasa anayependwa na wengi, lakini inaelekea hakufanikiwa kupata haiba hiyo. Wakazi wengi wa mji mkuu, na hata miongoni mwa wanachama wengi wa SPD, kila mara hawakuvutiwa sana na mtindo wake wa kupitisha maamuzi ya kisiasa. Wanapinga hasa jinsi alivyohusika na kashfa ya shuguli za benki na jinsi chama-tawala SPD kinavyozidi kudidimia sifa yake chini ya uongozi wake kutokana na kura ya maoni.
Gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU, linazingatia kashfa nyingine inayomkabili Gavana wa benki kuu ya Ujerumani Ernst Welteke, kwa kuandika: Katika mstari wa mbele, Ernst Welteke si mtu mwenye tabia rahisi. Hayo yanashuhudiwa na kashfa inayomkabili ya kukubali kulipiwa gharama za hoteli ya anasa na benki ya binafsi Dresdener Bank mjini Berlin, ambayo hadi sasa hakiri kwamba alifanya kosa kukubali mwaliko wa benki hiyo mwanzoni mwa mwaka wa 2002.
Kuhusu mada hii gazeti la OFFENBACH POST, linatoa maoni karibu sawa linapoandika: Ukweli wa mambo ni kwamba, jinsi wenye nyadhifa za juu wanavyozidi kuimarika katika mamlaka, hivyo ndivyo wanavyozidi kupoteza hisia zao za uadilifu. Kwa mishahara yao minono na marururupu ya kila aina, hawachoki katika kutaka makuu na maisha ya anasa. Kwa sababu hii waendeshaji mashtaka wamefungua kesi dhidi ya gavana huyu wa benki kuu mjini Frankfurt. Hatima yake bado haijulikani, hata baada ya uamuzi uliopitishwa jana na uongozi wa benki kuu kwamba, Ernst Welteke atenge kando kwanza kwa muda wadhifa wake. Lakini serikali mjini Berlin, hairidhiki, bali kinyume chake inamtaka ajiuzulu kabisa wadhifa wake.
Nalo gazeti mashuhuri la magharibi mwa Ujerumani RHEINISCHEPOST, katika uhariri wake linatahadharisha juu ya uwezekano wa kufanyika mashambulio ya kigaidi wakati wa sherehe za siku kuu za Pasaka, kwa kuandika: mahali ambapo panahatarishwa hasa ni mji wa Roma, kwa sababu magaidi wa kiiislamu wana mpango wa kuiadhibu Italia, kwa sababu ya kutuma wanajeshi nchini Irak, na pili kwa sababu mashambulio dhidi ya sherehe za kanisa katoliki mjini Roma, yangekuwa ishara muhimu kwao kimataifa. Kitisho hiki kinatukumbusha onyo lililotolewa na idara ya upelelezi ya marekani CIA, kwamba Baba Mtakatifu asiendeshwe sala zake hadharani wakati wa Pasaka bila ya kuvaa mavazi ya usalama na kuhutubia akiwa ndani ya gari lisiloweza kuvunjwa na mabomu wala silaha za aina nyingine.
Onyo hili linatokana na ukweli kwamba, kiongozi wa Kanisha katoliki, anapinga ulinzi wa kila aina, anapendelea kuwa katikati ya waumini wake. Hakubadili msimamo wake, hata baada ya jaribio la kumuua la kigaidi mwaka la mwaka 1981, ambalo alinusurika kwa majeraha.