Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
13 Aprili 2004Gazeti mashuhuri la hapa jijini Bonn, GENERAL-ANZEIGER, kuhusu hatima ya maofiwa wawili wa ulinzi wa mpakani wa Ujerumani, waliotekwa nyara nchini Irak, na ambao wanahofiwa huenda ikawa wameshauliwa, linauliza: Je, ni kitu gani ambacho maofisa hao wawili wamefanya kuwaudhi WaIrak? Hakuna chochote. Walikuwa tu safarini ya kawaida kuelekea ubalozi wa Ujerumani kwa ajili ya kubadilishana zamu. Kwa waasi wa Irak, ni sawa kama wanawaua au kuwaruhusu kubakia hai mateka wao. Kuhusiana na mkasa huu, inabidi kukumbukwa tu kwamba, Ujerumani ilikuwa mojawapo ya nchi ambazo zilipinga kwa kila njia vita katika Irak, lakini iliwabidi baadhi ya wasaidi wake wa ujenzi upya kuihama Irak kwa sababu ya ukosefu wa usalama.
Nalo gazeti la mashariki mwa Ujerumani OST-THÜRINGER ZEITUNG, linachangia mada hii kwa kuandika: Shabaha ya makundi ya waasi sio tena ni mashambulio dhidi ya wanajeshi wa wakaliaji pekee, bali pia dhidi ya raia wa kigeni, ambao wamekwenda nchini humo wakiwa na malengo ya kiamani. Makaundi hayo ya waasi hayachagui, kwao kila mgeni hutazamwa ni agenti wa idara ya upelelezi ya kimarekani CIA.
NÜRNBERGIESCHE NACHRICHTEN linasisitiza: Matukio mapya nchini Irak, hapana shaka yanachafua sifa ya rais George W.Bush, hasa ikikumbukwa jinsi anavyokabiliwa sasa na mbinyo mkali. Siasa zake kuelekea Irak, zinadhihiri ni msiba badala ya ujasiri, hali ambayo Kansela wa Ujeqrumani pamoja na rais wa Ufaransa Gerhard Schröder na Jaqcues Chirac, hawakutaka kuhusika nayo. Harakati za Rais Bush za kupambana na ugaidi, zinazidi kukosolewa, kwa sababu hachukulii kuwa muhimu tahadhari mbele ya mashambulio mapya. Si hayo tu yanayomhangaisha Bush, bali pia kwa sababu ya kuzidi kuchafuka hali nchini Afghanistan. Na hayo yote miezi michache kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini mwake. Hakuna rais mwingine wa Marekani, aliyewahi kujibebesha binafsi matatizo chungu nzima katika siasa za nje, kuliko George W.Bush..
Gazeti mashuhuri la mji mkuu Berlin, TAGES-SPIEGEL, nalo linauliza, je, Irak imegeuka sasa ni Vietnam ya Bush? Kihistoria, naam. Vita vya Vietnam vilidumu miaka 18, na viligharimu roho za wanajeshi 58 000 wa kimarekani, achilia mbali wale waliojeruhiwa. Lakini wamerikani wanaweza kufurahi kwamba, wengi miongoni mwa raia wa Irak, hata ikiwa hawasemi wazi hadharani, wanafurahi kwamba dikteta wao aliyekuwa akiwakandamiza tangu miongo Saddam Hussein alitimuliwa. Ndio maana mtu anaweza kusema hakuna maasi ya kitaifa dhidi ya wakaliaji nchini humo.
Tukigeukia mada nyingine, tunakuta yale yanayoandikwa na gazeti la TRIERISCHE VOLKSZEITUNG, linapojishugulisha na msimamo wa vyama vya wafanya kazi vya Ujerumani kuhusu mpango wa mageuzi wa serikali, linapoandika:
Hadi sasa viongozi mashuhuri wa vyama vya wafanya kazi kama vile Sommer, Bsirske na wengineo, waliweza kutabasamu tu kwa sababu katika misimamo yao walifanikiwa kupinga kwa mafanikio malengo ya serikali ya muungano kati ya vyama vya SPD na Kijani. Hata hivyo, haya hayawezi kutazamwa kama ni mafanikio, kwa sababu wawakilishi hawa wa wafanya kazi hawakufanikiwa hadi sasa kutoa jawabu la kuaminika. Ndio maana mwenyekiti mpya wa chama-tawala SPD, Franz Münterfering, anawataja kwa haki wenyekiti wa vyama vya wafanya kazi ni viongozi ambao binafsi hawajui wanakoelekea.
Tunakamilishiwa uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, kwa yale yanayoandikwa na gazeti la LAUSITZER RUNDSCHAU, kuhusu mada hii: Kama ilivyokuwa hadi nsasa, mkakati muhimu wa vyama vya wafanya kazi, ni mashambulio dhidi ya waajiri na serikali. Tutashuhudia hayo karibuni tarehe mosi mei, siku ya wafanya kazi ya kimataifa. Lakini hadi hapo, viongozi wa shirikisho la vyama vya wafanya kazi, wako mbioni kujiandaa kuwatuliza wafanya kazi waliokatishwa tamaa. Wanaweza kupaaza sauti vizuri, lakini wanashindwa kuwaeleza kinaganaga wafanya kazi mweleko wao. Vyama vya kisasa vya wafanya kazi, hautoa majibu kwa malengo yao, lakini sio tu kupiga makelele kwenye maandamano barabarani.