Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
21 Aprili 2004Gazeti mashuhuri la biashara la mji wa magharibi Düsseldorf HANDELSBLATT, kuhusu tangazo hilo la waziri mkuu wa uingereza Tony Blair la kufanyiza kura ya maoni juu ya katiba mpya ya nchi wanachama wa umoja wa ulaya, linaandika: Kwa tangazo hilo, waziri mkuu Balir amechukua hatua itakayomwezesha kupumua, hasa kwa sababu sasa nchi yake Uingereza inaweza kuahirisha kura hiyo ya maoni hadi mwakani. Tangazo hilo limejibiwa kisiasa kwa namna mbali mbali katika nchi nyingine za ulaya, hasa kwa sababu ya wanasiasa kuwa na hofu ya uamuzi wa raia katika nchi zao. Makao makuu ya umoja wa ulaya mjini Brussels, yanabidi kukumbuka kwamba, hayawezi kutarajia mafanikio makubwa kwa sababu raia wengi wakiwemo wakulima, hawajui kinaganaga yaliyomo katika katiba hiyo.
Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER ALLEGEMEINE ZEITUNG, linatoa maoni: Waziri mkuu Blair amejitokeza ghafla jukwaani kusema kile alichokuwa akiwakilisha tangu muda mrefu,
nacho ni kwamba, katiba ya ulaya haitabadili hata kidogo msimamo wa Uingereza kuelekea umoja wa ulaya, ndio maana ni sawa kama kura hiyo ya maoni itaikubali katiba hiyo mpya au la.
Nalo gazeti la REUTLINGER GENERAL ANZEIGER, linamaanisha: Bw.Blair sasa ameweka kila kitu juu ya karata moja. Baada ya kukabiliana na wimbi la wengi nchini mwake la kupinga vita vya Irak vilivyoungwa mkono na Blair mwenyewe, waziri mkuu wa Uingereza sasa ananuwia kuokoa haiba yake kwa kufanyiza kura ya maoni.
Gazeti la mji wa Lüneburg, LANDES-ZEITUNG, linachangia mada hii kwa kuandika: Kwa tangazo hilo haimaanishi kwamba serikali ya London ingepoteza ushawishi wake katika umoja wa ulaya, lakini Uingereza ingekabiliwa na hali ya kutengwa. Ni kutokana na kura hiyo ya maoni pekee, ambapo waziri mkuu Blair angeweza kuwatuliza badhi ya raia nchini mwake ambao hawakubaliani na kushirikishwa nchi yao katika umoja wa ulaya.
Nalo gazeti mashuhuri la Kolon, KÖLNER STADT ANZEIGER, linazingatia mada nyingine kabisa, nayo ni ule uamuzi uliopitishwa na mahakama ya kikatiba ya Ujerumani kuhusu utozaji kodi sekta za kiuchumi zinazochafua mazingira – linaandika: Uamuzi uliopitishwa na mahakhama ya kikatiba ya Ujerumani, unamaanisha siasa za kodi zina kina kirefu cha uhuru wa kuchukua hatua binafsi, lakini wenye kushikilia hatamu za kisheria, wanaweza kuchangia kwa umbali fulani utatuzi wa swala hili. Lakini kama malengo ya uamuzi huo ni barabara, hili ni swala lingine kabisa.
Kuhusu mada hii gazetzi la mashariki mwa Ujerumani LEIPZIGER VOLKS-ZEITUNG, linaandika: Serikali ya Ujerumani inakaribisha uamuzi huo kama ni mafanikio, lakini sio namna mahakhama ya kikatiba ilivyochukua hatua ya kutipisha uamuzi huo. Sababu ni kwa kuwa, kutokana na mvutano wa sasa kuhusu utozaji kodi kwa jumla, uamuzi huo wa kutoza kodi kwa nia ya kuhakikisha usafi wa mazingira, hautakuwa rahisi kutekelezwa na serikali ya muungano kati ya vyama vya SPD na Kijani.
Tunakamilishiwa uchambuzi kutoka magazeti ya Ujerumani hii leo kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti lingine la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU, kuhusu mada hii, linakumbusha: utozaji kodi dhidi ya uchafuzi wa mazingira, haumaanishi chingine kuliko kodi ya mauzo. Wakati serikali ya zamani ya Kansela Helmut Kohl, ilipopandisha kodi ya mauzo mnamo miaka ya 90, pindi kuifanya michango ya malipo ya uzeeni kuwa madhubuti, hayo yalikuwa kwa mujibu wa katiba. Ndio maana hapa linazuka swali, je, kwanini utozaji kodi huo uwe ghafla hauambatani tena na kanuni za kikatiba baada ya miaka michache tu? Mahakimu katika Karlsruhe, kwa uamuzi wao, walibakia tu katika mkondo wao wa kisheria.