Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo:
22 Aprili 2004Kuhusu kuchaguliwa Gavana mpya wa benki kuu ya Ujerumani Axel Weber, gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG, linaandika: Kukomeshwa kwa kashfa ya gavana wa zamani wa benki kuu ya Ujerumani Welteke, kunatoa matumaini mazuri kwa wakati ujao. Kuchaguliwa kwa mtaalamu huyu wa mambo ya uchumi Weber kushikilia wadhifa wa mtangulizi wake Welteke, ni uamuzi wa busara. Ukweli wa kwamba serikali ya Ujerumani imeamua kuachilia mbali dai la kutaka kukabidhiwa wadhifa huo katibu wa dola, ambaye hana maarifa mengi juu ya ulinzi wa thamani ya sarafu, unadhihirisha kwamba, serikali inaheshimu uhuru wa benki kuu wa kuendesha shuguli zake bila kuingiliwa.
Gazeti la mashariki mwa Ujerumani OST-THÜRINGISCHE ZEITUNG, linachangia mada hii linaposisitiza: Prof.Axel Weber kutoka chuo kikuu mjini Kolon, anajulikana si mtu anayeelemea sana upande wa siasa, bali yeye ni mtaalamu mwenye kipaji cha kuongoza shuguli za pesa na uchumi.
Kipaji chake hapana shaka kitakuwa ni mchango muhimu wa kuokoa haiba ya benki kuu. Na hapana shaka maarifa yake makubwa kuhusiana na siasa za namna ya kushikia usukani shughuli za pesa, kutapiga jeki maendeleo ya benki kuu ya Ujerumani na benki kuu ya umoja wa ulaya.
Gazeti la biashara la mji wa magharibi Düsseldorf, HANDELSBLATT, linatoa maoni: Wanasiasa waongozao katika Ujerumani wanakabiliwa na matatizo makubwa. Vyama vikubwa vya kisiasa vya umma, SPD,CDU na CSU, vilishindwa kupata wagombea wao wanoafaa kushikilia wadhifa huu mmojawapo wa juu kabisa katika Ujerumani. Tangu karibuni, ilizuka hali katika Ujerumani kwamba, nyadhifa za juu za dola, ziliwaangukia wataalamu ambao hawapo katika vyama vya kisiasa. Tutoe mifano miwili: Baada ya vyama-ndugu vya upinzani vya CDU na CSU, kumpendekeza ofisa wa hadhi ya juu, ambaye hakujulikana sana hadharani, Horst Köhler, kushikilia wadhifa wa rais mpya wa Ujerumani, nayo serikali ya muungano kati ya vyama-tawala SPD na Kijani, vimemkubali mtaalamu na professa huyu wa shuguli za kiuchumi na fedha Axel Weber, kushikilia wadhifa wa gavana mpya wa benki kuu ya Ujerumani. Bila kujali nyadhifa zao, wataalamu hawa wawili wanashuhudia namna isivyo kweli kila mara kushikiliwa nyadhifa za juu za dola na wataalamu kutoka vyama vya kisiasa.
Tugeukie mada nyingine kabisa: Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Wolfgang Clement, ameeleza wasiwasi kuhusu sheria ya kuwaruhusu wenye maduka katika Ujerumani kufungua biashara zao kwa muda mrefu zaidi kila siku. Kati ya maswala mengine waziri Clement anataka kupigwa marufuku biashara za maduka mnamo siku za jumapili. Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la Kolon, EXPRESS, linaandika: Kwa pendekezo lake la kubatilishwa sheria kuhusu muda wa kufunguliwa maduka kila siku katika Ujerumani, waziri wa uchumi Clement anazingatia ukweli wa mambo. Yaani, hapana dalili yoyote inayodokeza kwamba, serikali ingekuwa mwamrishaji wa wenye maduka ni kuanzia saa ngapi hadi saa ngapi kila siku wanaruhusiwa kuuza bidhaa zao. Isitoshe, waziri wa uchumi haoni ushuhuda wowote wa kuhalalisha kufunguliwa maduka katika stesheni za magari moshi siku za jumapili, lakini sio maduka ya jirani ya mjini. Huu si ufuataji wa haki sawa. Bora ingehakikishwa hali ya kumruhusu mwanabiashara kuamua binafsi ni kwa muda gani anataka kufungua duka lake, kwa mfano, hadi masaa ya usiku.
Tunakamilisha uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la kusini mwa Ujerumani STUTTGARTER ZEITUNG, kuhusu mada hii, linasema: Waziri wa uchumi Clement ana destri moja aliyokwishazoea, nayo ni utangazaji wa malengo yake badala ya kuchukua hatu. Alianza destri hii tangu alipokuwa waziri-mkuu wa mkoa wa magharibi wa North-Rhein Westfalia, na bado anaendelea nayo. Haonyeshi, kwa mfano, namna ya kupunguza urasimu mwingi, kama anavyoshikilia. Kwake ingekuwa bora kutangaza au kuzingatia maswala machache ambayo ni rahisi kutekeleza, badala ya kutangaza mambo ambayo ni shida kuwahakikishia wanauchumi na wanabiashara.