Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo
21 Juni 2004Gazeti la kusini mwa Ujerumani STUTTGARTER ZEITUNG, kuhusukukubaliwa katiba mpya ya umoja wa ulaya na mkutano wa kilele mjini Brussels linamaanisha lengo hasa la katiba hiyo bado halijafikiwa, linapoandika: Mtungo uliokubaliwa sasa wa katiba hiyo mpya ya umoja wa ulaya, utabidi kufanikiwa kwanza kuruka viunzi vya kitaifa mnamo miezi ijayo, yaani kama itakubaliwa na raia wa nchi zilizo wanachama kwa njia ya kura ya maoni, ambayo itaweza kuifanikiwa tu, iwapo raia wa nchi zote 25 watafahamishwa wazi wazi malengo yake ya kisiasa.Lengo la kutanuliwa kwa umoja wa ulaya kwa nia ya kuimarisha ushirikiano wa karibu wakati ujao, linaweza kufanikiwa tu, iwapo utambulisho wa kitaifa na wa kimkoa utafahamiwa ni uzalendo unaoambatana na katiba hiyo.
Kuhusu mada hii, gazeti mashuhuri la Kolon, EXPRESS, linatoa maoni: Ijapokuwa yameshapatikana mafanikio makubwa miongoni mwa nchi wanachama, bara la ulaya bado liko mbali na nia ya kusimama juu ya jukwaa moja la kisiasa.
Haya yanashuhudiwa na mvutano unaoendelea kuhusu mteule rais mpya wa halmashauri ya umoja wa ulaya. Kwani mgombea anayependekezwa na nchi fulani, anapingwa ghafla na kundi la nchi nyingine. Tatizo lenyewe sio hasa ni kipaji cha mgombea, bali kinachotiliwa uzito hasa ni kujua mgombea huyo wa rais mpya anatoka kambi au chama gani cha kisiasa.
Nalo gazeti la mji wa mashariki wa Gera OST-THÜRINGISCHE ZEITUNG, linaeleza hofu kwamba, upinzani katika kura ya maoni ya kitaifa, huenda ukaifanya kushindwa katiba hii mpya. Lakini chombo hiki kinalipatia nafasi kubwa zaidi bara la ulaya kuimarisha msimamo wa pamoja wa kisiasa. Labda inafaa kuipatia nafasi kwanza kuthibitisha kwamba ni chombo kinachofaa kwa nchi zote za ulaya. Lakini kuna hofu kwamba katiba hii mpya huenda ikashindwa kwa sababu ya kukataliwa baadhi ya yaliyomo ndani yake na mabunge fulani ya kitaifa. Isitoshe, huenda katiba hii ikashindwa katika kura ya maoni kwa sababu ya raia kutoridhina na serikali katika nchi zao.
Mkuu wa benki ya posta ya Ujerumani, Klaus Zumwinkel, sasa anakumbwa na hali ya lazima ya kubuni mikakati mipya, baada ya huahirishwa mipango ya masoko ya fedha dhidi ya yale aliyokuwa akishikilia kwamba, mipango yote imeshakamilika. Kile kitakachokuwa kimuumiza kichwa hasa, ni ile tofauti ya bei zinazodaiwa katika hisa, kwa sababu huenda zikashuka tena. Kuhusu mada hii gazeti la kusini mwa Ujerumani SÜDKURIER, linaandika: Bila shaka meneja wa benki muhimu kama hii ya posta, ana haki ya kuuza tawi lake mojawapo kwa bei nzuri kabisa iwezekanavyo. Ijapokuwa hayo, inambidi mkuu huyu wa benki ya posta ya Ujerumani Zumwinkel, kukubali kwamba alichelewa kulichukulia hatua onyo la masoko ya fedha. Tangu majuma yaliyopita, wengi miongoni mwa wale walio na hisa, wanalalamika kwamba bei zake ni kubwa kupita kiasi.
Gazeti la OFFENBACH POST, linachangia mada hii linapouliza kwanza, je, kwanini mkuu Zumwinkel akachelewa kuchukua hatua ya kukupuza bei hizo za hisa? Hatua hii ya benki ya posta ya kuahirisha maamuzi kuhusu masoko ya fedha, ni sura mpya kabisa tangu kumalizika kipindi cha furaha ya kustawi kwa masoko haya miaka minne iliyopita.
Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani, kwa kutazama yalle yanayoandikwa na gazeti la mji wa kusini wa Munich, ABENDZEITUNG,
kuhusu mada hii: Wawekaji hisa ambao walikuwa wakidaiwa kulipa kiasi ya Euro 31.50 kwa kila hisa, wanahisi kudanganywa. Ikiwa sasa inawezekana kudai bei ya Euro 28 kwa kila hisa, mbona kiwango hiki hakikuwezekana majuma mawili yaliyopita? Endapo taasisi za fedha za kijerumani, hususan Benki kuu Deutsche Bank, hazitaacha kucheza kamari kuhusu bei za hisa, basi zitawavunja nyoyo waekezaji, na sio katika Ujerumani pekee.