Uhalifu waongezeka Bukavu na Goma tangu kutekwa na M23
13 Machi 2025Wakaazi wa miji hiyo ya Goma na Bukavu mashariki mwa Kongo wanaishi katika hofu kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na ujambazi hasa kutokana na kwamba waasi hao hawana idadi ya kutosha ya maafisa wanaoweza kulinda usalama wa raia maeneo hayo ambayo kwa jumla yanakadiriwa kuwa na zaidi ya raia milioni tatu.
Baadhi ya vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa takriban visa 10 vya mauaji huripotiwa kila siku huko Bukavu. Kitendo cha wafungwa kutoroka kutoka gerezani, lakini pia uwepo wa wapiganaji waliogeuka wahalifu, ni miongoni mwa sababu zinazozidisha tatizo hilo la ukosefu wa usalama.
Anne Marie Kwinja ni mkazi wa Bukavu na anaeleza jinsi maisha yalivyo chini ya utawala mpya wa waasi wa M23.
" Binafsi kama mkazi, mwanafunzi na mjasiriamali, hali kwa kweli si nzuri. Siwezi kutembea kwa uhuru kutokana na usalama mdogo, mauaji ya hapa na pale na hata uporaji. Nimebadilisha hata aina ya mavazi ili kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji wa kingono. Kwa sasa nalazimika kurejea nyumbani mapema, kabla ya saa kumi na mbili jioni. Majambazi wamekuwa wakiwavamia raia na kuwapora. Hali ni ya kutisha, hakuna mfumo wowote wa kisheria hapa Bukavu."
Soma pia: Maafisa wa Afrika kwenye UN waonya juu ya mzozo nchini Kongo
Wakati miji hiyo ya Goma na Bukavu ikianguka mikononi mwa waasi wa M23, silaha nyingi ziliachwa kiholela na jeshi la Kongo na washirika wao ambao ni wapiganaji wanaojiita Wazalendo, ambao walilazimika kuondoka kwa haraka. Silaha hizo hatimaye zilianguka mikononi mwa majambazi ambao wanahatarisha usalama wa raia huku M23 ikionekana kushindwa kulidhibiti suala hilo.
Awali, Bukavu lilikuwa jiji linalojulikana kwa shughuli zake za kiuchumi na kifedha, lakini kwa sasa hali ni tofauti kabisa, jambo linalochochea vitendo vya ujambazi. Benki Kuu ya Kinshasa bado haijaidhinisha kufunguliwa kwa benki, jambo ambalo pia linawazuia wakazi kuweza kutumia fedha walizojiwekea kama akiba.
HRW: Madhila ya wanahabari na wanaharakati Kongo
Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limeelezea madhila wanayopitia waandishi wa habari huko Kongo ikiwa ni pamoja na kushambuliwa, kuvamiwa majumbani, kupewa vitisho vya kuuawa na kuishi katika hofu.
Si waandishi wa habari pekee, bali pia wanaharakati wamekuwa wakilengwa na vitendo hivyo vinavyoendeshwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda. Mtafiti mkuu wa HRW Clementine de Montjoye amesema takriban wanaharakati 200 wameomba hifadhi tangu kuanza kwa mashambulizi ya M23 huko mashariki mwa Kongo.
(Vyanzo: DW,AFP)