Uhalali wa shambulizi la Israel kwa Iran wazua mjadala mkali
18 Juni 2025Israel imetetea shambulizi hilo kama la "kujilinda kwa tahadhari” dhidi ya kile ilichokiita mipango ya Iran kutengeneza bomu la nyuklia. Hata hivyo, sheria ya kimataifa inatambua tu haki ya kujilinda iwapo kuna mashambulizi yanayoonekana kuwa ya dharura na ambayo hayawezi kuzuiliwa kwa njia nyingine, kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Profesa Matthias Goldmann, mtaalamu wa sheria za kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha EBS, anasema mashambulizi hayo hayakukidhi vigezo vya kujilinda.
Goldmann pia anasema, "Kuna sharti la kuwepo kwa shambulizi la dharura ambalo haliwezi kuzuiwa kwa njia nyingine. Kutokana na ushahidi uliopo, hakuna dalili kuwa Iran ilikuwa karibu kufanya shambulizi hilo".
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), iliyotolewa siku moja kabla ya shambulizi hilo, Iran haikuwa ikishirikiana kikamilifu, lakini hakuna ushahidi uliooneshwa na Israel kuthibitisha kuwa Iran ilikuwa inapanga kufanya shambulizi la nyuklia hivi karibuni. Taarifa za kijasusi kutoka Marekani zinaonesha Iran ilikuwa bado iko nyuma miaka mitatu kufikia kutengeneza bomu la nyuklia.
Israel yenyewe ina silaha za nyuklia, ingawa haijawahi kuthibitisha rasmi, wala kutia saini Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Bado kunamipaka ya kisheria
Hili linazidisha ugumu wa hoja ya kwamba Iran ilikuwa tishio la dharura, hasa ikizingatiwa mfano wa Vita Baridi ambapo nchi mbili zenye nyuklia hazikutumia silaha hizo kwa hofu ya mashambulizi ya kisasi.
Kwa upande wa sheria ya vita, Profesa Tom Dannenbaum wa Fletcher Chuo cha Sheria na Diplomasia, anaeleza kuwa mara vita vinapoanza, bado kuna mipaka ya kisheria.
Naye Dannenbaum anataja mfano wa mashambulizi ya Israel dhidi ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran majumbani mwao na kusema kufanya kazi kwenye mradi wa silaha hakufanyi mtu kuwa mpiganaji.
Wakati huo huo, Iran pia imeshambulia maeneo ya raia mjini Tel Aviv, jambo ambalo linakiuka wajibu wa kuchukua tahadhari za kuyalinda maisha ya raia.
Licha ya mapungufu ya wazi, wataalamu kama Goldmann, Milanovic na Dannenbaum wanakiri kuwa kuna uwezekano mdogo wa kesi kama hizi kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ) au hata Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya.
Sababu kuu: migogoro hii huwa ya kisiasa mno na mara nyingi hutatuliwa kwa njia za kidiplomasia kuliko mahakamani.