Uhaba wa fedha Goma toka mji huo kutekwa na waasi wa M23
4 Aprili 2025Baada yakuteuliwa kwa kiongozi mpya wa Benki ya Akiba na Mikopo, CADECO, mwezi wa Machi, uongozi wa kundi la waasi la M23/AFC ambao umetwaa udhibiti wa mji huu wa Goma uliahidi kuanzisha huduma za kibenki ili kuwasaidia wananchi, lakini hadi sasa hilo halijatekelezwa huku wakaazi wa hapa wakiendelea kuhangaika.
Tayari baadhi ya shughuli za kibiashara zimesimama na mzunguko wa fedha kupitia benki umesita, hali inayowatia hofu maelfu ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo ili kujimudu kimaisha.
Kama ilivyo kwa raia wengine, Assani Murairi anaelezea baadhi ya changamoto zinazowakabili.
"Mimi pia nimeathirika na hali hiyo kama vile wengine. Kwa sasa imekuwa vigumu kuchukua pesa zangu nilizoziweka kwenye benki kama akiba na hilo ni tatizo kubwa kabisa. Tizama jinsi gani hakuna tena uhusiano kati ya Goma na mji mkuu, Kinshasa. Hatuna jinsi ya kutuma na kupokea pesa na hivyo kuathiri familia yangu", alielezea Murairi.
Uhaba wa dola za Marekani umechangia pia pakubwa kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali katika mji wa Gomauliochukuliwa na M23/AFC mapema mwanzoni mwa mwezi wa Januari.
Hali mbaya ya kiuchumi
Asubuhi kama vila mchana, mamia ya wananchi huvuuka mpaka kuelekea katika mji jirani wa Rubavu nchini Rwanda kutafuta hela kwenye benki, hali ambayo imekuwa ni tafauti ilivyokuwa kawaida. Kanyere ZUBEDA hana tena uwezo wa kufanya shughuli zake za kibishara.
"Ombi letu kuu kwa viongozi ni kufungua benki na hiyo itasaidia watoto wetu kupata amani na hata sisi kupewa mikopo. Hapa awali tulikuwa tukifaidika pesa elfu 50 za Kongo baada ya kuuza biashara zetu, lakini kwa sasa ni vigumu sana."
Pamoja na kuendelea kushuhudiwa kwa machafuko katika baadhi ya maeneo mkoani Kivu Kaskazini na Kusini, Dola 1 ya Marekani inabadilishwa sasa kwa Faranga za Kongo 3,200 badala ya 2,500 kama ilivyokuwa wiki wiki mbili zilizopita.
Akizungumza na DW, Dady Saleh, mchambuzi wa maswala za kiuchumi mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema hali ya kiuchumi itaendelea kuwa ngumu.
"Tatizo hilo linaeleweka kabisa sababu benki zinatumika na hiyo benki kuu mjini Kinshasa na kusema kweli benki inaonesha nguvu za taifa, lakini wakati huu M23 ikiudhibiti mji wa Goma hawana kabisa hiyo nguvu za kufungua huduma za benki."
Kuendelea kufungwa huko kwa milango ya benki katika majimbo ya Kivu kaskazini na Kusini kumeyatumbukizia majimbo hayo mawili katika hali mbaya ya kiuchumi, ambako sasa kunawafanya baadhi ya wakaazi kuazimika kuhamia katika mataifa jirani kusaka huduma hiyo muhimu kwa biashara na hata maisha.