Uhaba mkubwa wa chakula watishia wakimbizi wa Kakuma Kenya
20 Juni 2025Kwenye kambi ya Kakuma, wanawake kwa wanaume wamekusanyika kupokea nafaka na choroko za msaada. Kuanzia mwezi huu wa Juni, shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa chakula, WFP, limepunguza posho inayowapa wakimbizi hadi asilimia thelasini.
Hiki ni kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa kambini Kakuma. Kadhalika hela za mkononi walizotengewa wakimbizi zimesitishwa. Hilo limewawia vigumu wafanyabiashara wakimbizi wanaowapa bidhaa wenzao kwa mkopo. Claude Niyonzima mmiliki wa duka anakiri kuwa hali imekuwa ngumu.
"Watu wanakuja dukani wanasema najua unanidai lakini sijui vile ntakulipa. Huwezi kumfanya chochote. Ukienda kwake unaamua tu kumuacha. Tunachosubiri ni kama usaidizi mwengine utapatikana tuweze kulipwa vinginevyo Kazi itaendelea tu", alisema Niyonzima.
Makaazi ya Kalobeyei yaliyoko Kakuma yaliundwa kwa mfumo wa kuwapa wakimbizi hela za matumizi ila kwa sasa hakuna tena mfumo huo. Kika Ngakani mkimbizi kutokea Butembo, jimboni Kivu ya Kaskazini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo anaamini suluhu ni kujipanga upya.
"Tulikuwa na uzoefu wa kuchukua chakula dukani Kwa deni. Ukifika unalipa, tena unachukua deni lakini ilifika kiwango watu wa duka wanakwambia uko na deni huwezi kupata jengine. Bamba chakula nilikuwa nanunua nayo mchele, mafuta na makaa. Hivyo vitatu pekee. Kwa sababu familia yangu ni ya watu saba, nilikuwa nikibeba kilo hamsini za mchele,maharagwe na magunia mawili ya mkaa , naongezea na mtungi mmoja wa mafuta na ile alfu saba imeisha. Lakini sasa hivi haitakuwa!", alisikitika Ngakani akizungumza na DW Kiswahili.
"Akiomba akilipa anapata tena"
Kika ni mkulima na anasimamia kitalu cha mboga na pilipili kwa ufadhili wa shirika ka kijamii la Inkomoko linalowapa mikopo kadri ya uwezo wao wa kulipa. Elizabeth Kamwaro afisa wa ushauri wa biashara wa Inkomoko ana unga mkono kauli hizo.
"Sisi kama Inkomoko tunawashikilia kwa mafunzo na kuwapa mikopo ambayo inalingana na uwezo wa kulipa wa biashara. Na hatuwapi mara moja tu. Akiomba akilipa anapata tena. Kama hajui pa kupata bidhaa, sisi Inkomoko tuko kwenye kaunti nne hapa Kenya. Tunawaunganisha, muuzaji na mnunuzi kutoka Kakuma", alisema Kamwaro.
Hali ngumu kambini imesababishwa na wafadhili wa kimataifa hususan Marekani kupunguza kwa zaidi ya nusu mchango wao kwa miradi ya kibinadamu. Ufadhili huo ndio unaogharamia miradi ya Umoja wa Mataifa ya kuwasaidia wakimbizi. Kwenye hotuba yake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasisitiza kuwa wanyonge wanahitaji kushikwa mkono.
Utapia mlo kambini Kakuma na Dadaab umekuwa tatizo Kwa watoto na Kina mama wanaonyonyesha kwani umepita viwango vya dharura. Miradi ya WFP ya kuwahudumia wanaotatizwa na utapia mlo ililazimika kufungwa Mwaka 2024 kwasababu ya uhaba wa fedha.