Ugiriki yaimarisha sheria kwa waomba hifadhi waliokataliwa
4 Septemba 2025Hatua hiyo inadhihirisha msimamo mkali zaidi wa nchi hiyo dhidi ya wahamiaji, kufuatia ongezeko la wakimbizi waliowasili eneo la mipakani kusini mwa nchi hiyo mwaka huu.
Nchi hiyo ya bahari ya Mediterania ilikuwa mstari wa mbele wakati wa mgogoro wa uhamiaji wa mwaka 2015 hadi 2016, ambapo zaidi ya watu milioni moja waliokuwa wakikimbia vita na umaskini kutoka Mashariki ya Kati na Afrika walivuka kuelekea Ulaya.
Ingawa idadi ya wahamiaji ilipungua kwa muda, mwaka huu kumekuwa na ongezeko la watu wanaowasili kutoka Libya kupitia visiwa vya Crete na Gavdos hali iliyosababisha serikali kusitisha kwa muda upokeaji wa maombi ya hifadhi kutoka wahamiaji wa Afrika Kaskazini.
Sheria hii mpya inasemaje?
Sheria mpya inaeleza kuwa wahamiaji wasio na nyaraka wanaoingia kwenye eneo la kusini kabisa mwa Ulaya kutoka nchi ambazo Umoja wa Ulaya unazichukulia kuwa salama, na wasio na haki ya kupata hifadhi, watalazimika kurejea makwao au kuzuiliwa kwa angalau miezi 24 na kulipa faini inayoweza kufikia euro 10,000.
Hatua hii ni sehemu ya sera kali za uhamiaji za serikali ya kihafidhina inayoongozwa na Waziri Mkuu Kyriakos Mitsotakis, ambaye tangu achukue madaraka mwaka 2019 ameongeza ulinzi wa mipaka kwa kujenga uzio kaskazini na kuimarisha doria baharini ili kuzuia wahamiaji.
Waziri wa Uhamiaji, Thanos Plevris, aliliambia bunge siku ya Jumanne kwamba haki za Wagiriki wanaotaka kulinda nchi yao zinapaswa kupewa kipaumbele kuliko haki za mtu ambaye maombi yake ya hifadhi yamekataliwa na anaendelea kuishi nchini humo kinyume cha sheria.
Serikali ya Ugiriki tayari imewarudisha mamia ya wahamiaji
Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema sheria hiyo inaweza kuwaadhibu wahamiaji wanaohitaji ulinzi wa kimataifa. Limeshauri kuwepo kwa mchakato wa haraka wa kushughulikia maombi ya hifadhi ili kutambua mapema ni nani mkimbizi na nani siyo, na kuwashughulikia kwa usahihi.
Serikali ya Ugiriki imesema tayari imewarejesha mamia ya wahamiaji wasio na nyaraka, baada ya kusitisha maombi ya hifadhi mwezi Julai, na inapanga safari zaidi za ndege kuelekea Pakistan, Bangladesh na Misri mwezi huu.
Mashirika ya haki za binadamu yameishutumu Athens kwa kuwarudisha kwa nguvu waomba hifadhi kwenye mipaka ya bahari na nchi kavu, huku Shirika la Ulinzi wa Mipaka la Umoja wa Ulaya likisema mwaka huu linachunguza kesi 12 za madai ya ukiukaji wa haki za binadamu na Ugiriki.