Ugiriki yaonya kuizuia Uturuki kufikia mfuko wa ulinzi wa EU
24 Julai 2025Hayo yanatokana na mvutano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo jirani kuhusu nani ana haki katika Bahari ya Aegean, pamoja na haki ya uzalishaji wa nishati na usimamizi wa maswala ya uhamiaji ambayo ni mgogoro uliojitokeza hiyi karibuni.
Uturuki, ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO lakini si wa Umoja wa Ulaya, kisheria inayo haki ya kupata ufadhili wa fedha kwa ajili ya sekta ya ulinzi na pia ina haki ya kushiriki katika mipango ya ununuzi wa pamoja wa silaha kupitia mpango wa SAFE wa Umoja wa Ulaya wenye thamani ya euro bilioni 150, unaolenga kuimarisha uwezo wa kijeshi wa Ulaya na kupunguza utegemezi kwa NATO na Marekani.
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, amesema hawataruhusu ushiriki wa Uturuki katika mpango huo ikiwa itaendelea kutishia kuanzisha vita na kupinga mamlaka ya Ugiriki katika eneo la Aegean.
Uturuki imekuwa ikitishia vita iwapo Ugiriki itaamua kwa upande mmoja kupanua utawala wake katika Bahari ya Aegean.