Uganda yahamisha kesi ya Besigye katika mahakama ya kiraia
21 Februari 2025Mamlaka ya Uganda imesema kuwa imefutilia mbali azma ya kumshtaki kiongozi wa upinzani Kizza Besigye kwa uhaini katika mahakama ya kijeshi, na kuhamisha kesi hiyo katika mahakama ya kiraia, hatua ambayo imemfanya kusitisha mgomo wake wa kula.
Mwanasheria Mkuu wa Uganda Kiryowa Kiwanuka ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali imehamisha kesi zote zinazohusu raia, ikiwa ni pamoja na ile ya Besigye, kutoka mahakama za kijeshi hadi mahakama za kiraia kuambatana na uamuzi uliotolewa Januari 31 na mahakama ya juu nchini humo.Uganda: Besigye kuhukumiwa katika mahakama ya kiraia
Kiwanuka ameongeza kuwa kesi ya Besigye kwasasa iko mbele ya mahakama ya kiraia na sio ya kijeshi.
Wakili wa Besigye Ernest Kalibala, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Besigye leo alifikishwa katika mahakama ya kiraia Kampala kusikiliza mashataka mapya dhidi yake.
Wakili wake mwingine, Erias Lukwago, amepongeza uamuzi huo lakini akaongeza kuwa umepitwa na wakati.