Uganda yaafikiana na Marekani kuwachukua wahamiaji haramu
21 Agosti 2025Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Vincent Bagiire Waiswa, amesema katika taarifa kuwa makubaliano hayo ni ya muda na yenye masharti, ikiwemo kutowachukua watu wenye rekodi za uhalifu na watoto wasiokuwa na mlezi.
Waiswa ameongeza kwamba Uganda ingependelea kuwapokea watu wenye uraia wa Kiafrika chini ya makubaliano hayo. Tangazo la Kampala kuhusu makubaliano hayo linakuja siku moja baada ya nchi hiyo kukanusha kuwepo kwa makubaliano kama hayo.
Pia inajiri baada ya Rwanda kusema itapokea hadi wahamiaji 250 mapema mwezi huu. Kigali bado haijatoa maelezo zaidi ya makubaliano hayo, ambayo Washington haijathibitisha. Hata hivyo utawala wa Trump umefikia makubaliano na Sudan Kusini.
Trump alenga kuwafurusha mamilioni ya wahamiaji
Rais wa Marekani, Donald Trump analenga kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji wanaoishi nchini humo bila vibali halali, huku serikali yake ikilenga kuwapeleka wahamiaji hao katika nchi ya tatu, ikiwemo kuwapeleka wahalifu waliokwishahukumiwa nchini Sudan Kusini na Eswatini.
Utawala wa Rais Donald Trump umefanya mazungumzo kuhusu mpango wa kuwapeleka watu kama hao katika nchi za tatu, miongoni mwao zikiwa ni El Salvador na Eswatini, ambazo zimeshutumiwa vikali na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Uganda, Rwanda na Sudan Kusini wakubali kuchukua wahamiaji
Uganda ambayo inahifadhi karibu wakimbizi milioni 1.7, tayari imeelemewa ikilinganishwa na mataifa mengine barani Afrika, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa. Na ndiyo nchi ya karibuni zaidi ya Afrika Mashariki kutangaza makubaliano hayo na Washington, ikiungana na Rwanda na Sudan Kusini.
Umoja wa Mataifa unasifu sera za ukimbizi za taifa hilo linaloongozwa na Yoweri Museveni kwa karibu miongo minne sasa, zinazowafungulia milango waomba hifadhi.
Hata hivyo taifa hilo limeshuhudia ongezeko kubwa la watu wanaoingia nchini humo mwaka 2024 na hasa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, lakini pia machafuko nchini Sudan Kusini na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.