Uganda kupambana na habari potofu mitandaoni
4 Aprili 2025Serikali ya Uganda ilianza kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii miaka kumi iliyopita lakini hatua ya kupiga marufuku Facebook miaka mitano iliyopita wakati wa uchaguzi kilikuwa kilele cha mikakati yake ya kusudio lake.
Waziri wa TEHAMA, Habari na Mwongozo wa Kitaifa, Chris Baryomunsi, amebainisha kwamba wanaendelea kuwekeza katika teknolojia zitakazohakikisha udhibiti wa matumizi ya mitandao ya kijamii kufuatia malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali kwamba inatumiwa kueneza chuki na na uchochezi jambo ambalo linahatarisha umoja na usalama wa nchi.
"Hatutafungia mitandao ya kijamii kama Tiktok kama ilivyopendekezwa na viongozi fulani hivi karibuni ila tunawekeza katika njia ya kiteknolojia kuchuja taarifa ambazo tunadhani zinalenga kusababisha chuki na uhasama kwa hiyo lengo ni kudhibiti matumizi yake", alisema Baryomunsi.
Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wanataja hatua zozote za kubana matumizi ya mitandao ya kijamii kuwa hali ya kukiuka haki za watu kuwasiliana na kujieleza.
Wana mtazamo kuwa utawala unataka kutumia hila hiyo kufichia umma vitendo vyake vya kikatili kama ilivyodhihirika hivi majuzi katika uchaguzi mdogo ambapo wandishi habari na watu wengine walishambuliwa waziwazi na askari wa vyombo vya usalama katika kile walichokitaja kuwa jaribio la kubadilisha matokeo ya uchaguzi huo kumpelea mgombea wa chama tawala cha NRM.
Marufuku ya Facebook
Hofu na mashaka ni kwamba kufuatia tamko la Waziri ina maana kuwa hali itakuwa mbaya zaidi kuhusiana na matumizi ya mitandao ya kijamii kuelekea uchaguzi mkuu wa 2026. Hivi karibuni watu kadhaa waliodaiwa kuitumia mitandao hiyo vibaya wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka na hata wengine hawajulikani waliko.
Mwaka 2021, mtandao wa Facebook ulipigwa marufuku. Hadi sasa ungali hauruhusiwi rasmi ila watu huufikia kupitia mfumo wa kukwepa malipo wa VPN. Waziri amelezea kwa nini hadi sasa Facebook haijaruhusiwa tena:
"Tumendelea kuifungia Facebook maana ilidhihirisha kupendelea upande mmoja kulingana na jinsi ilivyokuwa ikuruhusu matumizi yake."
Jambo la kushangaza ni kwamba wizara na mashirika ya serikali yameendelea kutumia Facebook kuwasilisha taarifa zao ikishangaza ni hadhira gani wanalenga kuwasiliana nayo.
Wakati huo huo, mwendelezo wa mkuu wa majeshi Jenerali Muhoozi Kaineragaba mwanawe rais Museveni kusambaza taarifa zinazosababisha kero na ghadhabu ndani na nje nchi haukosolewi na utawala na Waziri amekwepa kutoa tamko kuhusu suala hilo alipoulizwa na wanahabari.